Content on this page requires a newer version of Adobe Flash Player.

Get Adobe Flash player

Historia ya Wizara
Wizara hii ni moja ya Wizara kongwe katika muundo wa Serikali tangu Uhuru mwaka 1961. Jina na muundo wake vimekuwa vikibadilika. Baada ya Uhuru Mwaka 1961 hadi mwaka 1972 Wizara hii ilikuwa ikiitwa Wizara ya Kazi, Mawasiliano na Ujenzi.

Kati ya mwaka 1972 na 1984 ilibadilishwa na kuitwa Wizara ya Kazi na Ustawi wa jamii. Kuanzia mwaka 1984 hadi 1987 ilibadilishwa tena na kuitwa Wizara ya Kazi na Utumishi. Mnamo mwaka 1987 muundo wa Wizara ulibadilishwa na kuitwa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo.

Mwaka 1990 hadi 2000 jina lilibadilishwa na kuitwa Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana. Hata hivyo mwaka 2000 muundo wake ulibadilishwa tena na kuitwa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo hadi ilipofika mwaka 2005 ambapo muundo huo ulibadilishwa na kuitwa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, mwaka 2010 jina lilibadilishwa tena na kuitwa Wizara ya Kazi na Ajira baada ya kuondolewa Idara ya Maendeleo ya Vijana.

Wizara ya Kazi na Ajira ina Idara nne, ambazo ni Idara ya Usimamizi Kazi na Huduma za Ukaguzi, Idara ya Huduma za Ajira, Idara ya Utawala na Utumishi na Idara ya Sera na Mipango. Aidha Wizara ina vitengo vya Fedha na Uhasibu, Ukaguzi wa Ndani, Msajili wa Vyama Huru vya Wafanyakazi na Waajiri, Habari, Elimu na Mawasiliano na Kitengo cha Ununuzi na Ugavi.

Vilevile Wizara inasimamia shughuli za mashirika na taasisi zifuatazo:- Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), NSSF, Shirika la Tija la Taifa (NIP), Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya jamii (SSRA).