Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

KAZI SACCOS YAFANYA MKUTANO MKUU WA SABA, MKOANI DODOMA


*Chama hiko kimejipanga kuongeza wanachama zaidi

*Kimejipanga kuwekeza kwenye vyanzo ambavyo vitasaidia kuinua mtaji Chama

Chama cha Ushirika, Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu (Kazi SACCOS) kimefanya mkutano wake mkuu wa tano wa mwaka 2020 Mkoani Dodoma.

Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Mtaa wa Reli, Novemba 28, 2020.

Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bi. Felister Shuli ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu alieleza kuwa vyama vya ushirika ni njia pekee ya kumkomboa mwanachama ili awaze kupata huduma za kimsingi, hivyo muunganiko huo ambao huwakutanisha watu mbalimbali unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha ushirika huo pamoja na wanachama wanatimiza malengo yao kwa pamoja.

“Familia yenye furaha inaanza katika muunganiko huu ambao unalenga kuwezesha wanachama kujiinua kiuchumi wa wenyewe na jamii inayowazunguka,” alieleza Shuli

Aliongeza kuwa, wanachama wanufaika kupatiwa mafunzo ya ushirika, ujasiriamali na stadi za biashara ili waweze kuwa wabunifu katika kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuinua mtaji wa ushirika wa Kazi SACCOS.

Aidha, Mkurugenzi huyo alipongeza uongozi wa Kazi SACCOS pamoja na wanachama kwa kuona umuhimu wa kuvialika vyama vingine kwenye mkutano huo ili waweze kujifunza namna vyama vingine vya ushirika vinavyotekeleza majukumu yao.

Akiongea katika Mkutano huo Mrajis wa Mkoa wa Dodoma Bw. Revocatus Nyagiro aliwaasa viongozi wa Kazi SACCOS pamoja na Saccos zote nchini kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni na pia kuheshimu na kusikiliza wanachama wa vyama hivyo vya ushirika.

Alieleza kuwa, mwelekeo wa Serikali ni kuimarisha vyama vya ushirika kwa muktadha huo wanachama inabidi watambue wanaanzisha vipi bidhaa mpya ambazo zitahamasisha wanachama kwa kuzingatia ushindani uliopo sasa katika sekta ya fedha.

Sambamba na hayo, amewahimiza viongozi na wanachama wa Kazi SACCOS kuendelea kufanya mikutano mikuu mara kwa mara ili kuimarisha chama hicho.

Awali akitoa taarifa ya Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mwenyekiti wa Kazi SACCOS Bw. Omar Sama amesema kuwa lengo la mkutano huo ilikuwa kutoa taarifa kwa wanachama kuhusu shughuli mbalimbali za chama pamoja na kuweka makisio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha ujao na mipango ya utekelezaji.

Mara baada ya mkutano huo viongozi wa Kazi SACCOS pamoja na wanachama walitembelea eneo ambalo linamilikiwa na chama hiko cha ushirika lililopo Mtumba, Jijini Dodoma na wanachama hao walipata fursa ya kujionea viwanja vinne (4) ambavyo vinaukubwa wa mita mrada zaidi ya 4,000.