Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

TEKNOLOJIA YA KITALU NYUMBA KUWAKOMBOA VIJANA


Serikali imejipanga kuboresha upatikanaji wa ajira kwa vijana nchini kupitia teknolojia ya kilimo cha kisasa (Green house).


Hayo yamesemwa hivi karibuni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama alipofanya ziara Mkoa wa Songea na Iringa ili kuhamasisha na kukagua maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kujenga vitalu nyumba (Green house) kwenye Mikoa hiyo.


Waziri Mhagama alisema kuwa Serikali imeamua kuanzisha mradi huo ili kuhakikisha vijana wanafikiwa kwa idadi kubwa na kuwawezesha kupata ujuzi na ajira kupitia teknolojia ya kilimo cha kisasa itakayowawezesha kujipatia kipato.


“Teknolojia hii itawawezesha vijana kulima katika eneo dogo, kupata mazao kwa wingi na kuweza kuyauza, vilevile kutumia eneo hilo kuweza kuajiri vijana wengine kwani asilimia zaidi ya 60% ya watu wanaojiajiri na kujishughulisha inatokana na na mashamba.” alisema Mhagama


Ameongeza kuwa vijana watafundishwa teknolojia hiyo ya kilimo cha kitalu nyumba ili iwawezeshe kuongeza thamani ya mazao watakayozalisha.


Aidha, Waziri Mhagama aliziagiza halmashauri zote kujipanga haraka katika utayarishaji wa miundombinu kwenye maeneo hayo na kuhakikisha vijana wanaandaliwa mapema pamoja na kuanzishiwa Vyama vya Ushirika (AMCOS) kwani wananchi wapo tayari kuona mradi huo unaanza kufanya kazi mapema.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bi. Christina Mndeme alishukuru Serikali kwa kuuweka Mkoa wa Ruvuma kuwa miongoni mwa mikoa itakayonufaika na mradi huo na kumhakikisha Mhe. Waziri kusimamia na kusambaza ujumbe kwa vijana ambao ndio walengwa.


“Tutahakikisha tunashirikiana kwa pamoja kuanzia ngazi ya mkoa, halmashauri hadi kitongoji katika kusimamia na kutunza maeneo yatakayokuwa na mradi huu, kwa kuwa mradi huu utakuwa na misingi ya kuongeza uchumi, kuleta ajira na kuongeza uzalishaji wa mazao hapa mkoani Ruvuma”


Waziri Mhagama alifanya ziara hiyo mkoani Iringa katika Halmashauri ya Mufindi na mkoani Ruvuma katika Halmashauri ya Songea Mji na Songea Vijijini, mradi huo unategemea kuanza kwenye Mikoa 7 ikiwemo ya Ruvuma, Iringa, Mwanza, Simiyu, Kagera, Manyara, Lindi.