Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

VIJANA 4200 NCHINI KUNUFAIKA MRADI WA KILIMO KUPITIA KITALU NYUMBA


Vijana takribani 4200 hapa nchini wanatarajia kunuafaika na kilimo kupitia mradi wa kitalu nyumba(green house), ambao utaanza kutekelezwa katika mikoa sita ambayo imekuwa kinara kwa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana, ukiwemo mkoa wa Simiyu na Halmashauri zake zote sita.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi ,Vijana Ajira na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu yenye lengo la kukagua maeneo ya ujenzi wa vitalu nyumba na uwepo wa maji yatakayotumika katika kilimo cha umwagiliaji.

Mvunde amesema katika kutekeleza mradi huo vijana watawezeshwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili iwe sehemu ya ajira yao, ambapo vijana watafundishwa kulima kwa tija kupitia kitalu nyumba na kujua namna ya kutengeneza vitalu nyumba na wananchi wengine wanapohitaji kujifunza namna ya kutengeneza vitalu nyumba wajifunze kwao.

“Tutaleta green house (Kitalu nyumba) ambayo itafungwa hapa na vijana wataelekezwa kulima kupitia huko, lakini pia tutawaunganisha na chama cha Wauza mboga Tanzania kwa ajili ya kutengeneza masoko ya uhakika ili green house (kitalu nyumba) hizo ziwe na tija” alisema Naibu Waziri Mavunde

Akiwa katika ziara yake Naibu Waziri huyo amekutana na baadhi ya vijana ambao watatekeleza mradi huo na kuwapongeza kwa uamuzi waliochukua na akatoa rai kwa vijana wote nchini kuachana kukaa vijiweni na badala yake wajishughulishe na teknolojia hiyo ili waondokane na umasikini.

Akiwa wilayani Busega, Bariadi na Itilima Mavunde ameeleza kuridhishwa kwake na maeneo yaliyotengwa na akatoa wito kwa viongozi wote kuwalea vijana wote watakaoanza kutekeleza mradi huo ili mradi huo uweze kuwa endelevu na uweze kuwaletea tija.

Mkuu wa Mkoa wa Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru Serikali kwa mpango huo ambao utawasaidia vijana kujiajiri kupitia vitalu nyumba na akamhakikishia Naibu Waziri kuwa mkoa wa Simiyu utahakikisha vijana wanafanya vizuri katika mradi huo

Mkuu wa wilaya ya Itilima amesema pamoja na vijana wilayani humo kujiandaa na mradi wa kilimo kwa kutumia kitalu nyumba Wilaya hiyo pia imeweka mpango wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na ufundi stadi yatakayowawezesha kupata maarifa ya namna ya kufanya shughuli za ujasiriamali na ufundi kama ajira zao.

Kwa upande wao vijana watakaofaidika na mradi wa kitalu nyumba wamesema wanaupokea mradi huo kwa mikono miwili na wakaomba Serikali iwasaidie kupata mikopo ili waweze kununua vifaa vya kisasa hususani mashine na zana za kilimo zitakazowawezesha kutekeleza mradi huo.

“Mradi huu sisi vijana tunaupokea kwa mikono miwili ombi letu kwa serikali tusaidiwe mikopo itakayotuwezesha kupata mtaji utakatufanya vijana tunufaike na kilimo, tupate vifaa bora kama mashine za kumwagilia na zana nyingine za kilimo ili tuweze kulima kisasa” alisema Matogolo Samwel kutoka Mwanyili wilayani Busega.

Katika ziara hiyo Mavunde ametembelea Halmashauri ya wilaya ya Busega, Halmashauri ya Mji wa Bariadi katika viwanja vya nane nane Nyakabindi na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima makao makuu ya Wilaya Lagangabilili.