Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI OFISI YA WAZIRI MKUU


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amefungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi yake upande wa Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu uliofanyika mapema mwishoni mwa wiki hii.

Akifungua mkutano huo uliofanyiaka Machi 16, 2019 katika Ukumbi wa mikutano wa Magadu mkoani Morogoro waziri aliwataka watumishi wa ofisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na ubunifu ili kuendelea kuleta tija na utendaji wenye kuleta maendeleo nchini.

“Naamini mkutano huu unalenga kugusa maeneo yote ya utendaji kazi ikiwemo kubainisha changamoto, fursa na jinsi ya kujipanga ili kuongeza tija na ufanisi katika maeneo yetu ya kazi,”alisema Mhagama

Waziri aliwaeleza watumishi kuutumia mkutano huo kama chombo muhimu cha kuendelea kujadili na kuweka maazimio yanayotekelezeka kwa kuzingatia umuhimu wa chombo hicho kilichopo kisheria katika kusaidia watumishi wa umma.

“Tumieni mabaraza haya kama eneo muhimu la kujadili na kutoa mapendekezo juu ya kuboresha mazingira ya kazi ili kuendelea kuwa na weledi katika kutekeleza majukumu ya ujenzi wa Taifa,”alieleza Mhagama

Waziri aliongezea kuwa, matumizi sahihi ya mkutano huo ni kuona namna utavyosaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili Idara, Vitengo pamoja na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi hiyo na kuwa na maoni, ushauri na mapendekezo yanayotekelezeka ili kufikia malengo waliojiwekea kwa mwaka wa fedha ujao 2019/2020

Pamoja na hayo Waziri alipongeza utendaji wa watumishi wa ofisi yake hususan Idara ya Kazi, inayoshughulikia masuala ya vibali vya kazi na kuendelea kuboresha mifumo na mazingira wezeshi ili kuendelea ,kulinda mazingira ya kazi na ajira nchini.

“Pamoja na idara zote kuendelea kufanya vyema, kipekee naipongeza Idara ya kazi kwa mabadiliko mapya ya kiutendaji kwa kuzingatia ilikuwa Idara inayotupa shida hususani upande wa vibali vya ajira, tunashukuru kwa mageuzi makubwa yaliyofanyika katika Idara hiyo kwa kuwa na usimamizi mzuri na kulinda mazingira ya ajira na kuleta manufaa nchini,”alieleza Mhagama

Sambamba na hilo waziri aliwapongeza watendaji wa Ofisi kwa ujumla kwa nafasi zao kwa kuwepo na mafanikio makubwa ya kiutendaji pamoja na mchango wa kila mtumishi katika utoaji wa huduma bora bila upendeleo kwa wananchi wote kwa haki na usawa.

“Sina budi kuwapongeza kwani kila mmoja wetu ametimiza majukumu na kuwa na mchango mkubwa katika kutimiza majukumu ya serikali yetu kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020,”alisisitiza Waziri Mhagama.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Bw. Andrew Massawe aliahidi kuendelea kusimamia maagizo na ushauri wa waziri kwa watumishi wa ofisi yake ili kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika kuboresha mazingira ya utendaji kwa watumishi ikiwemo kuendelea kupambana na rushwa mahali pa kazi na kuzingatia haki na usawa kwa watumishi wote.

Aidha Katibu Mkuu aliongezea kuwa, uwepo wa mabaraza hayo ni kwa mujibu wa sheria na agizo Na. 1 la mwaka 1970 ambalo linaelekeza utaratibu wa kuundwa kwa mabaraza katika Taasisi na Ofisi za Umma kwa kuzingatia sheria mbalimbali za Kimataifa ikiwemo zile za Shirika la Kazi Dunia (ILO)

“Kwa kuzingatia lengo la kuanzishwa kwa mabaraza haya ni pamoja na kuona utekelezaji wa Bajeti za Ofisi zetu pamoja na kutoa mapendekezo katika kuboresha utekelezaji wa bajeti zetu za kila mwaka,”alisisitiza Massawe