Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA AKERWA NA SEKTA BINAFSI YA ULINZI KUONGOZA KWA MIGOGORO MAHALA PA KAZI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameiagiza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, kuweka mpango Maalum wa kuhakikisha migogoro katika sekta binafsi ya Ulinzi haizalishwi tena kwa wingi kwani inasababisha kutumika vibaya kwa rasilimali muda kati ya mwajiri na Mfanyakazi hali inayopelekea kuchelewesha Maendeleo.



Waziri Mhagama amebainisha sekta nyingine zinazoongoza kuwa na migogoro mahala pa kazi kuwa ni Sekta ya Ujenzi na Sekta ya Elimu. Aidha, ameitaka Tume hiyo kufanya utafiti kwa sekta zote zinazoongoza kwa migogoro ya kikazi ili kubaini chanzo cha migogoro hiyo na kuandaa Mkakati Maalum wa kuishughulikia.

Mhagama ameyasema hayo leo mjini Morogoro tarehe 14 Januari, 2019, wakati wa kikao cha Baraza la wafanyakazi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kilichowakutanisha Wasuluhishi na waamuzi wa migogoro ya kikazi nchi nzima.

“Hii sekta Binafsi ya Ulinzi kwa nini huko migogoro haiishi? Nataka mpango wa kumaliza migogoro hiyo, shirikianane na Taasisi nyingine muweke mpango maalum utakao weza kutatua na kuhakikisha haizalishwi mogogoro mingine” Alisisitiza Mhagama.

Mhagama alifafanua kuwa Serikali ya Awam ya Tano inayoogozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiriakwa vitendo vya kupiga vita uzembe, ubadhirifu na vitendo vyote Vya rushwa mahala pa kazi.

“Nisisitize kazi ya Usuluhishi na Uamuzi ni kazi ya heshima na pia ni kazi ya wito. Hivyo wekeni mkazo kwenye suala la Usuluhishi ili kupunguza muda na mlundikano wa mashauri, pia bainisheni sekta nyingine zenye migogoro mikubwa. Elimu ni vyema iendelee kutolewa kwa Wadau kuhusu Sheria za Ajira na mahusiano kazini.” alieleza Mhagama.


Awali akiongea katika Mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Shanes Nungu alibainisha kuwa Tume hiyo itatekeleza maagizo hayo kwa kuboresha Mkakati Wa Mpango kazi Wa Tume ili kuwa na mpango mkakati kwenye mtazamo Wa kupunguza migogoro na unaolenga kumaliza migogoro kwa nataka katika sekta zinazoongoza kuwa na migogoro mahala pa kazi.

“Tumekuwa tunajitahidi kumaliza na kuipunguza migogoro ya kikazi, kwani tumefanikiwa kumaliza migogoro hiyo kwa asilimia 80 kwenye hatua ya Uamuzi na asilimia 77, kwenye hatua ya Usuluhishi” alieleza Nungu.

Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo kimefanyika kwa mujibu wa Agizo la Rais Na.1 la mwaka 1970. Baraza hilo huiwezesha Tume kuboresha Huduma na masuala ya utatuzi Wa migogoro ya kikazi kwa njia ya Usuluhishi na Uamuzi.