Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA- VIJANA TUMIENI FURSA ZILIZOPO NCHINI KUANZISHA VIJIWE VYA KIUCHUMI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao kwa kuanzisha vijiwe vya kiuchumi.



Kauli hiyo ameitoa na Waziri Mhagama wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo na miradi ya vijana iliyopo katika Kituo cha Maendeleo ya Vijana, Sasanda kilichopo Kata ya Nyimbili, Mkoani Songwe.



Akiwa katika ziara hiyo Mhe. Mhagama alieleza kuwa, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeendelea kutimiza azima yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, hivyo vijana watumie fursa hiyo kujifunza mambo muhimu na kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawafanya wabadilishe vijiwe wanavyokaa kuwa vya kiuchumi.



“Tunataka kuona vijana watakapo jifunza kilimo bora, ufugaji wa ng’ombe au nyuki wataweza kuboresha thamani mazao na bidhaa kwa kuanzisha viwanda vidogo ndani ya Mkoa wa Songwe, mkakati wetu katika kituo hiki ni kutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana kuongeza thamani ya mazao na bidhaa watakazozalisha ambazo zitakuwa ni kichocheo muhimu katika kufikia maendeleo yao” alisema Mhagama



Aliongeza kuwa, Takribani vijana 500 kwenye kituo hicho wamejifunza stadi za maisha, ufundi na elimu mbalimbali zinazotolewa kwenye kituo ambazo zitawawezesha kujipatia kipato.

Sambamba na hilo, Mhe. Mhagama aliwahimiza Viongozi wa Mkoa kushirikiana na Ofisi yake ili waweze kuwasaidia vijana ambao wamekwisha anzisha viwanda vidogo vidogo ndani ya mkoa huo kwa kuwawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuwatafutia soko la uhakika ndani na nje ya nchi.



Aidha, Waziri Mhagama alitoa rai kwa vijana kujiunga kwenye vikundi ambavyo ni endelevu na vyenye muelekeo wa kuanzisha viwanda vidogo vitakavyowawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao na pelekea kufikia uchumi wa kati kama mpango wa maendeleo wa taifa unavyoelekeza.

Pia, aliwaelezea juu ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo zitafanyika katika Mkoa huo na kuwataka vijana na wanawake kutumia fursa hiyo kuutangaza vyema mkoa wa Songwe.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi alieleza kuwa kituo cha Maendeleo ya Vijana cha Sasanda kimewawezesha vijana kujitambua na kujiwekea malengo ya maisha na kuyatekeleza kwa faida yao, jamii na taifa kwa ujumla.

“Tunatarajia kuanzisha mafunzo na programu zitakazowaelekeza vijana masuala ya kilimo biashara ambacho kitasaidia upatikanaji wa malighafi zitakazokuwa zinahitajika kwenye viwanda vilivyopo nchini,” alisema Kajugusi



Naye Bw. Silia Kibona ambaye ni mnufaika kupitia kituo hicho, aliishukuru Serikali kwa kuwajengea mazingira ya kujifunzia ambayo yamewasaidia kupata mafunzo muhimu na aliwahamasisha vijana wenzie kuhudhuria mafunzo yanayotolewa kwenye kituo hicho.

Kituo cha Maendeleo ya Vijana – Sasanda kilianzishwa mwaka 1979 kwa ushirikiano wa Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni wa Taifa, Vijana na Michezo iliyopo wakati huo pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Uanzishaji wa Kituo hicho ulifuatia kuanzishwa kwa mpango wa kuunda vikundi vya vijana vya uzalishaji mali, uliolenga kuwawezesha vijana wasio na ajira kuweza kujiunga na kufanya kazi za kujitegemea hasa katika sekta ya kilimo.