Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Kamati ya Bunge yaitaka CMA kutoa Elimu Maeneo ya Kazi


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeitaka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu Sheria za Kazi ili kudumisha mahusiano mema kazini na kuzuia migogoro isiyo ya lazima.

Maelekezo hayo yametolewa Oktoba 13, 2026 jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Regina Malima, wakati Kamati ilipokuwa ikipokea taarifa ya mwenendo wa utatuzi wa migogoro ya kazi kwa mwaka wa fedha 2024/25 hadi Septemba 2026.

Dkt. Malima amesema utoaji wa elimu ya kutosha kuhusu sheria za kazi utasaidia kupunguza migogoro sehemu za kazi nchini. Aidha, Kamati imeishauri CMA kushirikiana kwa karibu na vyama vya wafanyakazi ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia walengwa kwa haraka na kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Eveline Munisi, amesema Serikali imepokea mapendekezo yote ya Kamati na itayafanyia kazi kwa lengo la kuboresha utendaji na kuimarisha ufanisi wa mfumo wa utatuzi wa migogoro ya kazi. Pia aliishukuru Kamati kwa ushirikiano na usimamizi wake thabiti.

Awali, akiwasilisha taarifa hiyo, Mkurugenzi wa CMA, Mpulla Nashon, amesema kumekuwa na mwenendo mzuri wa usajili wa mashauri, usuluhishi, utoaji maamuzi na utekelezaji wake, huku akiipongeza Kamati kwa usimamizi mzuri.

Amesema vipaumbele vya Tume kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ni pamoja na kuboresha utoaji huduma kupitia Mfumo wa e-Utatuzi, ambao umerahisisha upatikanaji wa huduma, kupunguza mlundikano wa mashauri na kuongeza ufanisi kwa ujumla.