News
Tanzania kushiriki maonesho ya 26 ya wajasiriamali wadogo na wa kati Kigali
Tanzania inatarajia kushiriki Maonesho ya 26 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakayofanyika jijini Kigali, Rwanda, kuanzia Oktoba 30 hadi Novemba 8, 2026.
Maonesho hayo yanalenga kutoa jukwaa kwa wajasiriamali kuonyesha bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kupanua wigo wa biashara, kuongeza ujuzi na kutafuta masoko ya bidhaa na huduma zao.
Kaulimbiu ya maonesho hayo ni “Kuendeleza Mnyororo wa Thamani katika Sekta ya Ngozi na Kilimo cha Bustani (Matunda na Mboga) katika Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.”
Maonesho hayo yanafanyika kwa kuzingatia maamuzi ya Mkutano wa 48 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI), uliofanyika jijini Arusha Juni 4, 2026.
Maonesho hayo yanatarajiwa kuwa fursa kwa wajasiriamali wa Tanzania kutangaza bidhaa na huduma zao, kuimarisha mitandao ya kibiashara na kutafuta fursa mpya za masoko katika ukanda wa Afrika Mashariki.
