Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Kamati ya Bunge kukagua mgodi wa Geita


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imewasili mkoani Geita kwa ziara ya kikazi ya kukagua uzingatiaji wa sheria na miongozo ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Akizungumza wakati wa kikao cha mapokezi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita (Septemba 22, 2026), Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Dkt. Evaline Munisi, amesema kamati hiyo inabeba jukumu kubwa na la msingi katika kuhakikisha ustawi wa Watanzania wa kada zote.

Dkt. Munisi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake inatekeleza miradi kwa ufanisi kutokana na ushauri na maelekezo ya kamati hiyo, hatua inayochangia kufanikisha maono ya Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Alexander Mnyeti, amewakaribisha wajumbe hao na kuipongeza kamati kwa kazi nzuri ya kuisimamia Ofisi ya Waziri Mkuu na akaongeza kusema shughuli za uchimbaji madini mkoani humo zinaendelea kwa amani na usalama.

"Geita ina viwanda na migodi mingi, hivyo tunapendekeza safari nyingine mfike tena ili tuwapangie maeneo mengine mkajionee hali halisi ya uchimbaji na kutushauri ipasavyo kwenye maeneo yenye changamoto," alisema Mnyeti.

Kamati hiyo inaongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Hawa Mchafu, na inatarajiwa kutembelea na kukagua Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).