News
Vijana wapatiwa ujuzi kumudu ushindani soko la Ajira
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kuimarisha jitihada za kuwajenga vijana wa Kitanzania kiujuzi ili kumudu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchini.
Aidha, Mafunzo hayo yaliyofanyika leo Mei 20, 2026 wakati wa maandalizi ya mahojiano yanayoendeshwa na Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA), Jijini Dar es Salaam, yamewakutanisha vijana waliomaliza vyuo vikuu na vyuo vya kati wakiwa na dhamira ya kujifunza mbinu mbalimbali zitakazowawezesha kufanya vizuri katika mahojiano ya kazi.
Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa wamepata maarifa na mbinu muhimu zinazowajengea kujiamini, uwezo wa kujieleza kwa ufasaha pamoja na namna ya kujibu maswali ya usaili kwa ufanisi, jambo linaloongeza nafasi ya kufanikiwa kupata ajira.
Akizungumza Mhitimu wa fani ya Aircraft Engineering, Catherine Mollel, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kutambua namna bora ya kujibu maswali kwa ufasaha na kwa kuzingatia hoja kuu bila kupoteza muda.
“Nimejifunza namna ya kujibu maswali moja kwa moja bila kupoteza muda kwa maelezo yasiyo na msingi. Hii imeniongezea ujasiri mkubwa,” amesema Catherine.
Kwa upande wake, Seif Ndege, mhitimu wa Mechanical Engineering, amesema kushiriki mafunzo hayo kumemsaidia kupata mbinu mpya za kukabiliana na changamoto alizowahi kukutana nazo katika mahojiano ya awali ya kazi.
Washiriki hao wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuratibu fursa za ajira na kuweka mazingira wezeshi yanayowaandaa vijana kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Mafunzo hayo yanaelezwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za Serikali za kupunguza pengo kati ya elimu na ajira, huku yakichangia kuongeza ushindani, ujuzi na mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa.
.jpeg)

