Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

RAIS DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AZINDUA KIWANDA CHA BIDHAA ZA NGOZI CHA KILIMANJARO


* Apongeza PSSSF na Magereza kwa uwekezaji wenye tija

* Ataka kiwanda kikamilike na kianze uzalishaji kama ilivyokusudiwa

* Waziri Mhagama: Tumetekeleza maelekezo ya kuwekeza kwenye Viwanda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 22 Oktoba, 2020 amezindua kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro (Kilimanjaro International Industries Co. Ltd) kilichojengwa katika eneo la Gereza Kuu la Karanga, Moshi Mkoani Kilimanjaro kwa ubia wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF) na Jeshi la Magereza Tanzania.

Akizungumza na Wananchi waliohudhuria tukio hilo, Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa moja ya ahadi alizozitoa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015 ilikuwa ni pamoja na kujenga uchumi wa viwanda ambavyo vitatumia malighafi zinazopatikana hapa nchini na vyenye kuajiri watu wengi.

“Kuanzishwa kwa Kiwanda hiki cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro kumekuwa na manufaa mengi kwa Taifa ikiwemo kuzalisha ajira nyingi kwa wananchi, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni pamoja na kuongeza wigo na thamani ya soko la ngozi kwa wafugaji ,”

Alifafanua kuwa, kuna idadi kubwa ya Mifugo nchini itasaidia upatikanaji wa vipande vya ngozi katika kiwanda hicho kipya na cha teknolojia ya kisasa kilichoanza uzalishaji ambapo zaidi ya jozi Milioni 1.2 za viatu zitazalishwa kwa mwaka, soli za viatu jozi 2.1 na bidhaa mbalimbali za ngozi kama vile Mikanda, Mabegi, Pochi, Mikoba na Majaketi ngozi.

Alieleza kuwa kiwanda hicho kinahistoria toka mwaka 1978 ikiwa ni ndoto ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye aliamua kujenga kiwanda hicho ili kiweze kutengeneza viatu kwa ajili ya askari.

“Natambua Mkoa wa Kilimanjaro hauna mifugo mingi, mifugo ipo maeneo mengine lakini kwa kudhihirisha ndoto za Baba wa Taifa na kuwapenda wananchi wa Kilimanjaro, Serikali iliagiza kiwanda hiki kikubwa kijengwe hapa Kilimanjaro,”

Sambamba na hayo, Mhe. Rais, Dkt. Magufuli alipongeza Jeshi la Magereza kupitia Kampuni yao ya Prison Coorparation Sole kwa kufanyia kazi wito na ndoto za Baba wa Taifa katika kufufua kiwanda hicho. Pia aliupongeza Mfuko wa PSSSF kwa kuamua kuwekeza kwenye kiwanda hicho kilichopo Mkoani Kilimanjaro.

Aidha, Mhe. Rais, Dkt. Magufuli alitoa maagizo kwa Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha awamu ya pili ya ujenzi katika maeneo yaliyobaki na pia ameitaka kampuni ya TMC kutoka nchini ya Italia kukamilisha huo kwa muda uliopangwa. Pia alitoa wito kwa Jeshi la Magereza, PSSSF na Uongozi wa Kiwanda hicho kuhakikisha bidhaa zitakazozalishwa kiwandani hapo zinakuwa na ubora unaohitajika.

Akizungumza awali Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama alisema Ujenzi wa mradi huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais aliyoyatoa tarehe 9 Mei, 2016 wakati wa ufunguzi wa majengo ya vitega uchumi vya PSSSF na NSSF jijini Arusha ambapo alielekeza Mifuko kuwekeza zaidi katika viwanda badala ya majengo ili kukuza ajira na kuendeleza uchumi.

Kwa Upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. George Simbachawene alieleza kuwa Wizara yake kupitia Jeshi la Magereza litaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na PSSSF ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa katika kuanzishwa kiwanda hicho yanatimia.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA. Hosea kashimba alisema kuwa mradi huo umehusisha uboreshaji wa Miundombinu ya Kiwanda cha zamani, ujenzi wa kiwanda kipya ambao umegawanyika katika awamu mbili, moja ikihusisha uwekaji wa mitambo ya kutengeneza viatu pamoja na majengo ya ukataji, ushonaji, umaliziaji ambao umefikia 100% na awamu ya pili inahusu ujenzi wa kiwanda cha kuchakata ngozi, karakana na maabara ambao umefikia 50%.

Aliongeza kuwa Mradi huo unathamani ya Bilioni 136, Mfuko wa PSSSF unamiliki asilimia 86 na Jeshi la Magereza asilimia 14 huku Jeshi la Magereza likiwa limechangia eneo la kiwanda lenye hekari 25 (mita za mraba 100,000) pamoja na kiwanda cha zamani na Mfuko wa PSSSF unachangia gharama za ujenzi wa majengo, ununuzi wa mashine na mitambo pamoja na gharama za uendeshaji.

“Mpaka kukamilika kwake mradi huu unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 136 ikijumuisha gharama za ardhi, ujenzi wa majengo, mashine na mitambo, ushuru wa forodha na gharama za uendeshaji na mtaji wa kuendesha kiwanda,” alieleza Kashimba

Sherehe ya Uzinduzi wa Kiwanda hicho imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. George Simbachawene, Kamishna Jenerali wa Magereza Suleiman Mzee, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mghwira, Viongozi wa Dini na Watendaji Wakuu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.