Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

5875 Youth Benefit from Apprenticeship


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde, amesema hadi kufikia Juni mwaka huu vijana 5,875 wamenufaika na Mafunzo ya Stadi za Kazi kupitia vyuo 17 vya Don Bosco Net vilivyopo nchini.


Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo wakati wa mahafali ya vijana 988 waliohitimu mafunzo hayo kwenye Taasisi ya Don Bosco Jijini Dodoma.

Alieleza kuwa mafunzo hayo ambayo yanaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu yametolewa kwa vijana katika fani ya ufundi uwashi, ufundi magari, bomba, umeme, uchomeleaji, uwekaji terazo na marumaru, useremala, ushonaji nguo, mapishi, uchongaji vipuri, umeme jua.

Alifafanua kuwa kupitia Programu hiyo ya Ukuzaji Ujuzi nchini kati ya idadi vijana walionufaika na mafunzo ya uanagenzi ni 28,941, urasimishaji ujuzi ni 14,432, mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa vyuo vya kati na juu ni 5,975, kilimo cha kisasa kupitia teknolojia ya kitalu nyumba umwagiliaji kwa njia ya matone ni 8,980.


“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha tunafikia malengo ya kuwa na nguvu kazi ya vijana wenye ujuzi wa kutosha ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi na ustwai wa taifa lao," alisema Mavunde

Mavunde amesema vijana hao wengine wamepata kazi kwenye miradi mikubwa na waajiri wameendelea kupigana vikumbo kuhitaji vijana hao.

Hata hivyo, amesema serikali imeanza kuongea na wamiliki wa viwanda mbalimbali ili vijana hao wenye ujuzi wa fani mbalimbali waweze kuwa kuwa sehemu ya nguvu kazi itakayoongeza uzalishaji katika viwanda hivyo.


Naibu Waziri huyo amesema kuwa dira ya maendeleo ya Taifa inalenga ifikapo mwaka 2025, Tanzania ishindane na nchi zingine katika soko la dunia kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitakuwa zikizalishwa hapa nchini.

“Nguvu kazi yenye ujuzi stahiki inahitajika ili viwanda vitengeneze bidhaa zinazohitajika na zenye ubora, kutokana na umuhimu huo serikali imeamua suala la ukuzaji ujuzi wa nguvu kazi ya Taifa kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Taifa,”amesema.

Mavunde amesema Rais John Magufuli amechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kunakuwepo na nguvu kazi ya vijana wenye ujuzi wa kutosha.


“Serikali ina program nyingine inaitwa RPL ni mfumo wa urasimishaji wa ujuzi, kwa vijana wenye ujuzi ambao hawajapitia mfumo rasmi wa mafunzo ya ufundi, ukienda leo mtaani wapo vijana wanaojua kupaka rangi, kujenga, kutengeneza magari hawajawahi kusoma, serikali inachofanya inapeleka wakufunzi na kukaa na vijana hao kubaini mapungufu na kuwapa vyeti,”amesema.

Aliwataka vijana kuunda vikundi ili kupatiwa mikopo isiyo na riba kupitia fedha zinazotolewa na Halmashauri nchini na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Naye, Mkurugenzi wa Donbosco Net Tanzania, Father Merkades Lukanyaga, amesema mafunzo hayo ni ya miezi saba na yamefadhiliwa na serikali kwa asilimia 100 na yalianza mwaka 2019 na kampuni 900 zilitoa nafasi ya mafunzo kwa vitendo kwa vijana hao.


Amesema mafunzo hayo yanatolewa kwenye vituo 17 ambapo umewafikia vijana katika mikoa 13 Tanzania ambayo ni Dodoma, Singida, Iringa, Lindi, Ruvuma, Dar es salaam, Morogoro, Shinyanga, Geita, Kagera, Mara, Kilimanjaro na Arusha.

Kwa upande wake, Mmoja wa wahitimu, Elia Hargo, ameishukuru serikali kwa kuwafadhili vijana mafunzo hayo kwa maana yamekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha kushindana kwenye soko la ajira na pia ndoto walizokuwa nazo kama vijana zinatimia.