News
Maonesho ya Jua Kali fursa ya Kiuchumi kwa Wajasiriamali
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Zuhura Yunus amesema kuwa maonesho ya Jua Kali yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza masoko ya bidhaa za wajasiriamali na kuwawezesha kushiriki na kikamilifu katika uchumi wa kikanda.
“Tumeshuhudia kuimarika kwa ushirikiano wa kikanda umesaidia kuchochea ubunifu na kuendeleza minyonyoro ya thamani kwa biashara ndogo na za kati.” amesema
Amebainisha hayo wakati wa siku maalumu ya Tanzania katika Maonesho ya 25 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali yanayofanyika katika viwanja vya Uhuru Garden, Jijini Nairobi, Kenya.
Aidha, amesema kuwa Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilikubaliana kuwa na maonesho hayo kwa kutambua mchango wa sekta isiyo rasmi katika kukuza maendeleo ya nchi wananchama na imeendelea kutoa ajira kwa wengi, ambapo kwa Tanzania asilimia 29 ya watu wanaofanya shughuli za kiuchumi wanajishughulisha na sekta hiyo.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dkt. Bernard Kibesse akizungumza wakati wa hafla hiyo amewapongeza wajasiriamali wa Tanzania kwa bidhaa bora na amehimiza kuendelea kutumia maonesho hayo kama fursa ya kutengeneza masoko katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa bidhaa zinazozalishwa na wajasilimali.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (CISO -Tanzania), Lida Msaki ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha wajasiriamali zaidi ya 300 kushiriki katika maonesho hayo nchini Kenya.
Mwakilishi kutoka Burundi ambaye ni Mkurugenzi wa Forodha na Biashara kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kikanda, Ndizeye Bobby Jean, amewapongeza wajasiriamali wa Tanzania kuwa na bidhaa zenye ubunifu lakini pia amewahasa wajasiriamali wa jumuiya hiyo kuendelea kuwa wabunifu ili kuweza kufikia viwango vya kimataifa.
