Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

​Mhe. Katambi: Pensheni za kila mwezi kwa wastaafu zilishaboreshwa


Bunge limeelezwa kuwa hadi sasa wastaafu wote wa serikali wameboreshewa pensheni zao za kila mwezi ambapo ni tofauti na hapo awali.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameyasema hayo Septemba Mosi, 2023 bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum (CCM), Mhe. Nancy Nyalusi.

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji lini serikali itaboresha mafao ya wastaafu kwa kuongeza kiwango cha pensheni anayopata mstaafu kwa mwezi.

Akijibu swali hilo, Mhe. Katambi amesema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii huongeza kiwango cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu mara baada ya kufanya tathmini na kujua uendelevu wake na uwezo wa kulipa mafao kwa wanachama wake na kwamba tathmini hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kipindi kifupi, miaka mitano kwa kipindi cha kati na tathmini ya kipindi kirefu ni miaka kumi.

Amesema kanuni za ulipaji mafao Namba 11(1) za mwaka 2018 zilielekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuongeza pensheni kwa kuzingatia mfumuko wa bei na uendelevu wa Mfuko kila baada ya miaka mitatu.