Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Wadau Watakiwa Kusaidia Utekelezaji wa Mwongozo wa Utambuzi Watoto Wenye Ulemavu


Serikali imetoa rai kwa wadau kusaidia kuwajengea uwezo Waratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi ya Mama na Mtoto na Maofisa Lishe ngazi ya mikoa katika kutekeleza Mwongozo wa Taifa wa utambuzi wa mapema na afua stahiki kwa watoto wenye ulemavu.

Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ndio yenye dhamana ya kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa mwongozo huo.

Akifungua Kongamano la Afya kwa Viziwi Septemba 29, 2023 jijini Mbeya, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu kutoka ofisi hiyo, Rasheed Maftah, amesema hadi sasa Maofisa Ustawi wa Jamii na Maofisa Maendeleo ya Jamii wa mikoa nchini tayari wamepatiwa mafunzo ya utekelezaji mwongozo huo.

“Wizara ya Afya na wadau wetu Shirika la Afya Duniani (WHO) tunaomba mbebe jukumu la kuwajengea uwezo waratibu wa afya ya uzazi wa mama na mtoto namna ya kuweza kutekeleza mwongozo huu ili mtoto anapozaliwa apate na vipimo vya usikivu ili kuona hali yake ya kiwango cha usikivu na kama kuna dosari zozote afua stahiki ziweze kufanyika,”amesema.

Machi 16, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na watu wenye ulemavu Ikulu Chamwino mkoani Dodoma na kuelekeza kuimarishwa kwa mfumo wa utambuzi wa mapema wa watoto wenye ulemavu na kuwaunganisha na afua stahiki ili kuzuia au kupunguza makali ya ulemavu.