Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndalichako aridhishwa Maandalizi ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amekagua na kuridhishwa na shughuli za maandalizi ya Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 ambapo ameutaka Uongozi wa Mkoa wa Manyara kukamilisha miundombinu ya ujenzi wa uwanja wa Kwaraa kwa wakati ili kuruhusu shughuli za kilele kufanyika hapo Oktoba 14, 2023.

Ameyasema hayo Agosti 28, 2023 mkoani Manyara alipofanya ziara akiambatana na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Zanzibar, Fatma Hamad Rajab, ambapo wamefika Mkoani humo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya shughuli za kilele cha mbio za mwenge wa uhuru 2023 zitakazofanyika Oktoba 14, 2023 Mkoani humo

Prof, Ndalichako amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha zaidi ya shilingi Milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo na miundombinu nyingine kwa ujumla.

Ametoa wito kwa watanzania hususan mikoa ya Jirani kujitokeza kushiriki katika maadhimisho ya kilele cha mbio za mwenge wa uhuru ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, wamekagua uwanja wa Kwaraa yatakapofanyika maadhimisho hayo, Kanisa la Parokia Mtakatifu itakapo fanyika ibada ya Baba wa Taifa, uwanja wa stendi ya zamani itakapo fanyika wiki ya vijana na kukagua maendeleo ya vijana wa halaiki.

Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2023 zinaongozwa na kauli mbiu isemayo “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa viumbe hai na Uchumi wa Taifa”.