Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Mhe. Ndejembi ataka Matokeo Chanya katika Utendaji Kazi


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia masula ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watumishi wa Ofisi yake kuimarisha utendaji kazi ili kuleta matokeo chanya na yenye tija katika kuwahudumia wananchi.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema, Wananchi wanatarajia makubwa kupitia wizara hiyo ambayo inasimamia maeneo mbalimbali ikiwemo masuala ya maendeleo ya Vijana, Ajira, ustawi wa Watu wenye Ulemavu, Wafanyakazi, Waajiri na Wastaafu.

Amesema hayo leo Aprili 5, 2024 wakati alipowasili kwenye hiyo Ofisi iliyopo Mji wa serikali Mtumba kwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa Ikulu, Jijini Dar es Salaam tarehe 4 Aprili, 2024.

Vile vile, Mhe. Ndejembi amehamasisha menejimenti na watumishi wa Ofisi yake kuhakikisha wanasimamia maelekezo na miongozo yanayotolewa na viongozi wakuu wa serikali kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika utendaji kazi.

Kwa upande mwengine, Waziri Ndejembi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Waziri katika Ofisi hiyo na kuahidi kushirikiana na watumishi wa Ofisi yake ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na Serikali.

Akizungumza awali, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameahidi kutoa ushirikiano kwa Mhe. Waziri na Katibu Mkuu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Waziri Ndejembi amewasili katika ofisi yake ambapo alipokelewa na Naibu Waziri wa ofisi hiyo Mhe. Patrobas Katambi pamoja na Katibu Mkuu, Mhe. Mary Ngelela Maganga.