Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Mhe. Ridhiwani Kikwete ashiriki Mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Halmashauri ya Arusha Mjini


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameshiriki katika mapokezi ya mbio za Mwenge wa Uhuru Halmashauri ya Arusha Mjini, leo tarehe 11 Julai, 2025.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Kikwete amesema Mwenge wa Uhuru ni alama ya matumaini kwa wananchi pia ni jukwaa muhimu la kuwajengea vijana misingi ya uongozi wa taifa.

“Mbio za Mwenge wa Uhuru ni shughuli muhimu kitaifa, pia ni chombo cha kuwajengea vijana wetu uzalendo, maadili na maono ya kuongoza taifa hili,” alisema Mhe. Kikwete.

Ametoa pia wito kwa watumishi wa umma kuhakikisha wanalinda na kutunza miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa gharama kubwa za serikali, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na uendelevu wa miradi hiyo.

Baada ya mapokezi hayo, Mwenge wa Uhuru umeanza kukimbizwa katika Kata ya Muriet ambapo umezindua Mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Walimu katika shule ya Msingi TERRAT uliogharimu shilingi milioni 120 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri. Mradi huo upo katika hatua ya asilimia 90 ya utekelezaji.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndg. Ismail Ali Ussi, amepongeza utekelezaji wa mradi huo na kusema kuwa ujenzi wa miundombinu ya elimu ni nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo kwa jamii.