News
Ofisi ya Waziri Mkuu yawapatia mafunzo ya Ujuzi Wachimbaji Wadogo Chunya
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inaendelea kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini Chunya mkoani Mbeya, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wafanyakazi wa sekta ya madini kupata ujuzi, maarifa na stadi bora za kazi.
Mafunzo hayo yanatolewa kupitia programu ya Taifa ya kukuza ujuzi yenye lengo la kuimarisha uwezo wa wachimbaji wadogo wa madini kufanya kazi zao kwa ufanisi, usalama na tija zaidi.
Akizungumza Julai 8, 2025 wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Daudi Silasi amesema programu hiyo imekuwa na mafanikio makubwa katika Mikoa mbalimbali na sasa Mbeya ni miongoni mwa mikoa inayonufaika kwa awamu hii.
“Tunawapatia wachimbaji wadogo elimu na ujuzi juu ya usalama mahali pa kazi, matumizi sahihi ya vifaa, uhifadhi wa mazingira pamoja na mbinu bora za uchimbaji” amesema.
Programu hiyo imejikita katika mafunzo ya Uanagenzi (Apprenticeshiptraining), Mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa ujuzi, Mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa Wahitimu (Internship training) na Mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini.