News
Rais Mwinyi Ajionea Mifumo Mbalimbali Banda la Waziri Mkuu Sabasaba
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo tarehe 07 Julai, 2025 ametembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu lililopo katika Maonesho ya 49 ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Katika banda hilo, Dkt. Mwinyi ameona mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Taarifa za Watu Wenye Ulemavu (Persons with Disabilities Management Information System - PID-MIS) ambalo ni jukwaa la kidijitali linalotumika nchini Tanzania kwa lengo la kukusanya, kuhifadhi, kuchambua na kutoa taarifa sahihi zinazohusu watu wenye ulemavu.
Mfumo huu ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu katika kuhakikisha kuwa kundi la Watu wenye Ulemavu linatambuliwa, linapangwa vizuri na linapatiwa huduma stahiki kwa mujibu wa sheria, sera na mikakati ya taifa.
Vilevile alipokea maelezo kutoka kwa mtaalamu kuhusu Mfumo wa Ramani za Vihatarishi vya Maafa, ambao hutumia teknolojia ya mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS) kutoa taarifa muhimu kuhusu maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na majanga mbalimbali yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, kama vile mafuriko, ukame, na ongezeko la joto.
Rais Mwinyi ametembelea banda hilo wakati alipowasili katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya ufunguzi wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayofanyika Jijini Dar es Salaam.
Kauli Mbiu ya Maonesho hayo ni “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania.