News
Wachimbaji Wadogo wa Madini wapewa Ujuzi Mpya Mkoani Geita
✅ Naibu Waziri Kiruswa amesema Serikali Yajipanga Kuinua Sekta ya Madini zaidi.
✅ Mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi yaleta tumaini Jipya kwa Wachimbaji wa Madini.
Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa amefunga rasmi mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa wachimbaji wadogo wa madini 467 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Madini.
Akizungumza leo Julai 6, 2025 wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo, Mhe. Kiruswa amesema serikali ya awamu ya sita inaendelea kutekeleza mkakati wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kuongeza tija, usalama na ufanisi katika shughuli zao.
“Serikali imejipanga kuhakikisha sekta ya madini inakuwa kisasa zaidi, salama na inayozingatia sheria. Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi hizo na tunatarajia kuona mabadiliko chanya katika namna wachimbaji wanavyofanya kazi,” alisema.
Awali akizungumza Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Alana Nchimbi, amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 111.3 kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi tangu ilipoanzishwa mwaka 2016 na fedha hizo zimewezesha zaidi ya wanufaika 157,909 kupata fursa ya mafunzo yanayotolewa kupitia programu hiyo.
Aidha, amesema kwa Mwaka wa fedha 2024/25 Serikali ilitenga shilingi Bilioni 10.8 kwa ajili ya utekelezaji wa Programu hiyo ambapo jumla ya wanufaika 10,786 wamefaidika ikiwemo wachimbaji wadogo 479 wa Mkoa wa Geita.
Naye, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Geita, Bw. Titus Kabuo, ameshukuru serikali kwa kuendelea kuwa karibu na wachimbaji wadogo na kuwapatia mafunzo ya ukuzaji ujuzi.
Amesema juhudi za Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Madini zimeonyesha dhamira ya kweli ya kuwawezesha wachimbaji kufanya kazi kwa weledi na ubora.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa wiki mbili yaliwashirikisha wachimbaji wadogo zaidi ya 400 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Geita. Washiriki walipatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo kuhusu mbinu bora za utafutaji na uchimbaji wa madini.