News
Waziri Ridhiwani Kikwete asisitiza Ushirikiano wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kupitia ASSA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ametoa wito kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kupitia Jumuiya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Afrika (ASSA) kuendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuchochea maendeleo ya bara la Afrika.
Akizungumza wakati wa kikao cha majadiliano ya awali na wadau wa sekta ya hifadhi ya Jamii uliofanyika jijini Arusha tarehe 9 Julai, 2025, Mhe. Ridhiwani amesema kuwa kongamano hilo la Hifadhi ya Jamii na Maendeleo Shirikishi Barani Afrika linaongozwa na kauli mbiu isemayo “Sekta ya Hifadhi ya Jamii; Chachu ya Maendeleo ya Miundombinu kwa ajili ya masuala ya Kiuchumi na Kijamii katika Bara la Afrika.”
Aidha, amesema Jumuiya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Afrika (ASSA) inapaswa kuratibu na kuendeleza juhudi za pamoja katika kuimarisha na kuendeleza maendeleo ya miundombinu, ikiwemo kuanzishwa kwa Mfuko wa Miundombinu wa ASSA kwa Afrika ambao utaweka mifumo ya uwekezaji katika miradi ya miundombinu.
“Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania imeanza kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya miundombinu ikiwemo kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo viwanda, madaraja, makazi, pamoja na miundombinu mingine ya kijamii na kiuchumi,” amesema
Kwa upande mwengine, Mhe. Ridhiwani Kikwete amehamasisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kupitia Jumuiya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Afrika (ASSA) kuwekeza kwenye miradi yenye tija na manufaa makubwa kwa maendeleo ya Bara la Afrika, vile vile kuhakikisha maslahi ya wanachama yanakingwa.