News
Waziri Ridhiwani: Wekezeni kwa Maendeleo Kulinda Maslahi ya Wanachama
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ametoa wito kwa Mifuko ya Hifadhi ya jamii kuwekeza kwenye miradi ya Maendeleo huku kipaumbele kikiwa kulinda maslahi ya Wanachama wao.
Mhe. Ridhiwani ametoa wito huo wakati wa Mkutano wa 14 wa Kimataifa wa Watunga Sera wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Barani Afrika uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Amesema, katika kuimarisha usimamizi na uendelevu wa sekta ya hifadhi ya jamii, amezitaka mamlaka za mifuko hiyo kuhakikisha maamuzi ya uwekezaji yanazingatia vigezo vya uwazi, tija na ufanisi wa kiuchumi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo madhubuti ya usimamizi wa rasilimali za wanachama ili kuimarisha imani ya wananchi kwa mifuko hiyo na kuhakikisha ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Mifuko ya Hifadhi ya Jamii: Chachu ya Maendeleo ya Miundombinu na Ukuaji wa Kiuchumi na Kijamii Barani Afrika.”