Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Dkt. Munisi asisitiza ushirikiano katika kukuza stara na malezi bora kwa mtoto wa kike


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, ametoa wito kwa taasisi za dini, wazazi, walezi, waelimishaji na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu ya stara, kukuza maadili, kuimarisha malezi bora na kulinda ustawi wa watoto na wanawake nchini.

Dkt. Munisi ametoa wito huo Oktoba 25, 2026, jijini Dar es Salaam, alipomwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu katika hafla ya utoaji wa tuzo za Muslim Stara Women Awards, msimu wa kwanza, iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City.

Amesema kuwa, stara inapoambatana na elimu, malezi bora na tabia njema, humsaidia binti kujenga kujiamini, kuheshimu utu wake na kufanya maamuzi yenye busara. Ameongeza kuwa stara huchangia kukuza maadili na mahusiano yenye heshima katika familia, pamoja na kuimarisha utamaduni wa kuheshimiana, uwajibikaji na kuishi kwa amani katika jamii.

“Nitoe wito kwa taasisi ya Juby Enterprises Limited, taasisi za dini, wazazi, walezi, waelimishaji na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu ya stara, kukuza maadili, kuimarisha malezi bora na kulinda ustawi wa watoto na wanawake,” amesema Dkt. Munisi.

Akizungumza awali, Mkurugenzi wa Juby Enterprises Limited, kampuni iliyoandaa tuzo za Muslim Stara Women Awards, Juby Msuya, amesema tuzo hizo zimeanzishwa kwa malengo matatu makuu, ambayo ni kutambua mchango wa wanawake Waislamu wanaofanya vizuri katika biashara, elimu, uongozi, ubunifu na huduma za jamii; kuhamasisha mabinti kutambua uwezo wao wa kufanikiwa katika maisha ya kisasa huku wakizingatia misingi ya Uislamu; na kujenga mtandao wa kuwaunganisha wanawake Waislamu ili kusaidiana katika shughuli za biashara na maisha kwa ujumla.

Amesema tuzo hizo pia zinalenga kuwapa moyo mabinti kwa kuwaonesha kuwa wanaweza kufikia malengo yao katika nyanja mbalimbali za maisha huku wakidumisha misingi ya imani yao, pamoja na kuhamasisha ushirikiano na kusaidiana miongoni mwa wanawake Waislamu badala ya kushindana.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Prof. Alhad Mussa Salum, amesema utoaji wa tuzo hizo unaonesha juhudi zinazofanywa na wanawake katika kujenga taifa, huku wakizingatia stara kama jina la tuzo hizo linavyoakisi.

MWISHO