Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Dkt. Munisi ataka CWT na vyama vingine vya Wafanyakazi kuzalisha ajira


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, amevitaka vyama vya wafanyakazi nchini kuwekeza katika miradi ya kiuchumi itakayozalisha ajira mpya, akisisitiza kuwa mchango wao haupaswi kuishia katika kudai haki za wafanyakazi pekee.

Dkt. Munisi alitoa wito huo leo, Oktoba 16, 2026, jijini Mbeya, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wenyeviti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), yanayofanyika katika Ukumbi wa City Park.

Alisema vyama hivyo vina nafasi kubwa katika kukuza ajira nchini, akitolea mfano CWT ambayo imefanikiwa kuajiri watumishi 401. Aliwataka viongozi wa vyama hivyo kubuni miradi mipya na kuhakikisha ajira zinazozalishwa zinaripotiwa kwa mamlaka husika ili kutambua mchango wake katika uchumi.

Dkt. Munisi aliongeza kuwa vyama vinapaswa kuzingatia viwango vya usalama na afya mahali pa kazi vinavyosimamiwa na OSHA, kuchangia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na kufuata Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CWT, Mwl. Protas Magesa, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa chama wa kuwaimarisha viongozi wake. Alieleza kuwa mwaka 2026 chama hicho pia kimetoa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa, makatibu wa mikoa na wilaya, pamoja na walimu wenye ulemavu katika mikoa ya Dodoma, Iringa na Njombe.

Magesa alisema CWT pia imeendelea kushiriki katika vikao na wadau wa elimu, wakiwemo TUCTA, TEN/MET, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi ya Elimu Tanzania, TAMISEMI na Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi, kwa lengo la kuchangia maendeleo ya elimu nchini.