Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Katibu Mkuu Maganga Aongoza Ujumbe wa Tanzania Marekani Kuimarisha Usalama Kazini


Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Mary Ngelela Maganga, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika ziara ya kikazi nchini Marekani ambapo ujumbe huo ulikutana na uongozi wa American Industrial Hygiene Association (AIHA).

Katika kikao hicho leo Oktoba 22,2026 pande mbili zimejadili fursa za ushirikiano wa kimkakati kati ya AIHA na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), ikiwemo kuimarisha uwezo wa wakaguzi wa OSHA kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu katika ukaguzi wa afya na usalama mahali pa kazi.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Bi. Maganga amesema ushirikiano huo utaongeza ufanisi wa OSHA, kuimarisha utaalamu wa watumishi, kuboresha huduma za ukaguzi, upimaji na uchunguzi wa vihatarishi, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kisasa na matumizi ya teknolojia katika kudhibiti vihatarishi kazini.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo utajumuisha kujenga uwezo wa wakaguzi kupitia mifumo ya uthibitishaji wa umahiri, kushirikiana katika urekebishaji wa vifaa vya kupimia vihatarishi, pamoja na kuanzisha maabara ya kisasa nchini kwa ajili ya uchunguzi wa sampuli za mazingira ya kazi.

Katibu Mkuu Maganga aliambatana na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na OSHA.

Ziara hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kujenga uwezo wa kitaasisi wa OSHA, kwa lengo la kuhakikisha mazingira salama na yenye kulinda afya za wafanyakazi nchini.