News
Kisuo Aridhishwa Ubora Bidhaa za Ngozi KLICL, Apongeza PSSSF, Magereza Kukuza Ajira
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo amesema karidhishwa na ubora wa viwango vya bidhaa za ngozi zinazozalishwa na Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro (KLICL).
Amesema bidhaa hizo zinakidhi matakwa ya soko la ndani na zina uwezo wa kushindana katika masoko ya kimataifa sambamba na kuchangia ukuaji wa ajira na maendeleo ya uchumi wa taifa.
Mhe. Kisuo amebainisha hayo leo Januari 7, 2026 alipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda hicho kwa lengo la kukagua shughuli za uzalishaji, ubora wa bidhaa za ngozi zinazotengenezwa pamoja na mifumo ya uendeshaji wa kiwanda hicho.
*”Mradi huu ni chanzo cha Ajira ambapo unalenga kutoa Ajira 3,000 za kudumu, na Ajira zisizo za kudumu 4,000.”* amesema.
Aidha, amesema ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho unaonesha uwekezaji wenye tija unaofanywa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Fortunatus Magambo, amesema Mfuko una mpango wa kufanya upanuzi wa kiwanda hicho kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kuongeza fursa za Ajira kwa Vijana nchini.
