News
Kiwanda cha ngozi cha Kilimanjaro kuchochea fursa za ajira
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeridhishwa na maendeleo ya Mradi wa Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro (KLICL) na kueleza kwamba uwekezaji huo utachochea upatikanaji wa ajira pamoja na kuondokana na uagizaji wa viatu visivyo na ubora nje ya nchi.
Akizungumza Novemba 12, 2023 baada ya kukagua kiwanda hicho kilichopo Manispaa ya Moshi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia kwa dhati dhana ya uchumi wa viwanda na kwamba soko la ndani la viatu likiwa kubwa, uagizaji viatu kutoka nje ya nchi visivyo na ubora wa utapungua.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, ameahidi serikali itaendelea kufanyia kazi ushauri wa kamati kwa kuwa kipaumbele kikubwa cha Rais Samia ni kuleta ustawi wa watanzania.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Patrobas Katambi amesema suala la soko la viatu limeendelea kuimarika na kwa sasa kuna taasisi nyingi za serikali zinachukua viatu katika kiwanda hicho na mikakati ikiendelea kuhamasisha taasisi zingine kuchangamkia viatu hivyo ambavyo vina ubora unaotakiwa.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma(PSSSF), CPA Hosea Kashimba, amesema kiwanda hicho kinamilikiwa kwa asilimia 86 na mfuko huo, Jeshi la Magereza linamiliki asilimia 14 na uwekezaji wake hadi utakapokamilika unakadiriwa kufikia Sh. Bilioni 152.96.