News
Mafunzo ya Uanagenzi na Mkakati wa Uzalishaji Ajira Nchini
Katikati ya misitu ya miti ya mikorosho inayojulikana kama “dhahabu ya kusini”, katika mazingira yenye utulivu na hewa safi ya asili, ndipo kilipo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mtawanya kilichoanzishwa mwaka 1975 chini ya Wizara ya Elimu kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wananchi hususan vijana kwenye nyanja za ufundi stadi na malezi ya kuongeza ujuzi, kinachotoa matumaini mapya kwa vijana na wananchi wanaotafuta maarifa ya kujitegemea.
Mazingira hayo yanayoakisi utamaduni, uchapakazi na uchumi wa wakazi wa mikoa ya kusini, yanakifanya chuo hicho kuwa kitovu muhimu cha ukuzaji wa ujuzi, ubunifu na utaalamu wa kazi za mikono.
Kupitia mfumo wa mafunzo kwa njia ya uanagenzi na ufundi stadi, chuo hicho kimeendelea kuwa chachu ya kuwawezesha vijana kujiajiri, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na taifa.
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo Mtawanya, Mwalimu Sophia Mkopi akizungumza na mwandishi wetu (05 Mei 2026) ofisini kwake , alibainisha kuwa katika programu ya nane ya mafunzo 2025/26, kumekuwa na mahitaji makubwa ya vijana ambapo walipokea maombi zaidi ya 500 lakini kutokana na mgao wa Wizara walipatiwa vijana 100 kwa fani tano za ufundi.

Mwalimu Mkopi alitaja manufaa kadhaa ambayo wanafunzi wamepata kutokana na mafunzo ya Uanagenzi yanazodhaminiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano kwa mwaka 2025/26, ikiwa ni pamoja na:
Ujenzi wa miundombinu ya maji ambapo Wanafunzi wa fani ya ufundi bomba wameweza kusambaza mabomba ya maji kwenye majengo ya chuo hicho ikiwemo vyoo na hosteli .
Pili upatikanaji wa Bima ya Afya kwa Wanafunzi ambapo Serikali imeweza kutoa bima ya afya kwa wanafunzi wote kupitia fedha wanazolipa chuo hatua iliyongeza morali ya wanafunzi kujisomea na kusaidia wazazi kupunguza gharama.
Tatu, wanafunzi wameweza kupata ujuzi wa vitendo na nadharia katika fani zao kwa usimamizi wa wakufunzi kwa kuwa serikali serikali inatoa fedha za ununuzi wa vifaa vya mafunzo kwa wanagenzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya Wanafunzi wa Uanagenzi chuoni Mtawanya walieleza kuwa mafunzo wanayopata yamewasaidia kujenga ujuzi na kujiamini katika kazi za ufundi.
Jesca Albeto Mtonya (21), mwanagenzi wa fani ya ufundi bomba, alieleza namna mfumo wa umwagiliaji maji kwenye mashamba unavyofanyika kwa njia ya mabomba na ujuzi aliofundishwa hatua inayomsaidia sasa kufanya kazi ndogondogo.
Kwa upande wao wakufunzi akiwemo Sofia Hamis Lingondo, mkufunzi wa ufundi wa magari chuo cha Maendeleo Mtawanya, alisema kuwa programu ya Ukuzaji ujuzi imewasaidia vijana kupata ujuzi wa vitendo na nadharia katika fani zao.
"Mimi pia nilisoma hapa uanagenzi na kisha nikaenda kujiendeleza kwa ngazi ya juu kisha nimerejea na kuwa mkufunzi hapa Mtawanya," alisema Sofia akionesha manufaa ya programu ya Ukuzaji ujuzi kwa vijana.
Mratibu wa Mafunzo ya Uanagenzi chuoni hapo Kelvin Ndunguru alisema idadi ya vijana 100 wa kozi ya muda mfupi imekuwa na mchango kwenye maboresho ya chuo kwani kupitia mafunzo ya vitendo vijana (live projects) wameweza kutekeleza kazi za ufundi bomba, uchomeleaji na ufundi magari.
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi. Programu hii inalenga kuhakikisha kuwa nguvukazi ya Taifa letu inapata ujuzi stahiki ili iweze kujiajiri na kuajiriwa ndani na nje ya nchi, pamoja na kupunguza nguvukazi iliyo katika soko la ajira isiyo na ujuzi stahiki.
Katika Awamu ya Nane ya mafunzo inayoendelea katika vyuo 46 nchini, jumla ya vijana 5,746 wanapatiwa mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi kwa njia ya Uanagenzi nchini.

.jpeg)

