Habari

NAIBU WAZIRI AOMBA WANAOTUMIA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI KUENDELEA KUTUMIA

NAIBU WAZIRI AOMBA WANAOTUMIA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI KUENDELEA KUTUMIA

WATANZANIA wanaotumia dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi wametakiwa kuendelea kutumia pasipo kuacha, ili waweze kuishi maisha yenye afya iliyoimarika hivyo kuendelea kulitumikia taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mh. Antony Mavunde wakati akifungua kongamano la Kisayansi la uwasilishaji wa matokeo ya tafiti za UKIMWI nchini kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani mwaka 2018 linalofanyika katika Hoteli ya Morena mjini Dodoma.

Alisema kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 hadi 64 ambao walitoa taarifa kuwa wanatumia dawa za kufubaza VVU, asilimia 87.7 ndio wamefubaza VVU ambapo wanawake ni asilimia 89.2 na wanaume ni asilimia 84.

“Napenda kuhamasisha watanzania wote wanaotumia dawa za kufubaza VVU waendelee kuzitumia pasipo kuchoka na kwa kufanya hivyo wataweza kuishi maisha yenye afya iliyoimarika na furaha na hivyo kuendelea kulitumia taifa vyema” alisema

Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ni Pima VVU, Jitambue Ishi ambayo inaonesha ushahidi kutokana na matokeo ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI wa mwaka 2016/2017 hapa nchini.

Alisema utafiti huo unaonesha kuwa kama nchi bado hatujafanya vizuri katika kutimiza malengo 90 ya kwanza ya kimataifa yaani asilimia 90 ya WAVIU nchini wawe wamepima na kujua hali zao ifikapo mwaka 2020.

Mavunde alisema matokeo yameonesha ni asilimia 52 tu ya WAVIU nchini wanajua hali zao.

“Hii ina maana kwenye eneo la kupima kuna vikwazo vingi vinavyowafanya watu hasa wanaume kutojua afya zao, pengine nchi bado hatujapata ufumbuzi bado kwani kutokana na matokeo ya utafiti huo ni asilimia 45 tu ya WAVIU wanaume wanajua hali zao” alisema

Alisema katika kutekeleza tisini ya pili yaani asilimia 90 ya WAVIU wajuao hali zao wawe wameanza dawa za ARV ifikapo mwaka 2020 kama nchi, imepiga hatua japo kwa kusuasua kidogo kwa upande wa wanaume.

Alisema utafiti wa mwaka 2016/2017 umeonesha kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri kati ya miaka 15 hadi 64 ambao wanajua hali zao za maambukizi asilimia 90.9 walianzishiwa dawa za kufubaza VVU, wanawake wakiwa asilimia 92.9 na wanaume ni asilimia 86.1.

Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI, inaahidi kutoa ushirikiano.

Alisema malengo hayo ni pamoja na kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2023 kama ilivyobainishwa kwenye mkakati wa nne wa taifa wa kudhibiti UKIMWI nchini na hatimaye kufikia malengo ya sifuri tatu ifikapo mwaka 2030.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi na Mwakilishi wa UNAIDS nchini, Dk. Leo Zekeng alisema Tanzania imepiga hatua kubwa kupambana na UKIMWI tangu miaka ya 1980 na kwa upatikanaji wa tiba tangu mwaka 2010 na misaada ya pamoja kutoka serikalini, mashirika ya kiraia yanayowakilisha watu wanaoishi na VVU pamojka na mashirika ya kimataifa ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa.

“Tanzania inaweza kufikia lengo la kumaliza UKIMWI kama tishio la afya ya jamii kwa mwaka wa 2030 kama sehemu ya Malengo ya millennia na maono ya maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025” alisema

Alisema hadi sasa kwa bahati mbaya bado vikwazo vingine vya kupima VVU vinaendelea,

“Unyanyapaa na ubaguzi bado unaendelea huwazuia watu wasijaribu kuopima VVU na kujua hali zao, tunahitaji kukomesha unyanyapaa na ubaguzi katika mazingira yote hasa katika mazingira ya huduma za afya katika jamii yetu.” Alisema

Alisema upimaji wa siri wa VVU bado ni suala lenye wasiwasi, watu wengi bado hujaribu kupima baada ya kuwa na dalili za ugonjwa.

“Habari njema ni kwamba kuna njia nyingi za kuimarisha upatikanaji na upimaji wa VVU miongoni mwa wengine kuwa, kujipima, upimaji wa jamii husaidia watu kujua hali yao ya VVU” alisema

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko alisema kongamano hilo pia litaazimia mikakati mahususi itakayotoa matokeo zaidi katika kufanikisha dira ya kuwa na Tanzania isiyokuwa na UKIMWI kufikia mwaka 2030.

Alisema katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya UKIMWI duniani wamepanga kuzindua mkakati wa nne wa taifa wa kudhibiti UKIMWI (2018/2019- 2022/2023).