Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Naibu Waziri Katambi afafanua taratibu zinazofuatwa mtumishi akijifungua mtoto njiti


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema Mkataba wa Kimataifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na.183 kuhusu haki ya uzazi unaelekeza nchi wanachama kuweka utaratibu wa kuwalinda mtoto na mama kutokana na changamoto za uzazi ikiwemo kuzaa mtoto njiti.

Naibu Waziri Mhe. Katambi amebainisha hayo leo Novemba 11,2022 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum Zainabu Katimba aliyehoji

Je, ni lini marekebisho ya Sheria yataletwa Bungeni ili mwanamke anayejifungua mtoto njiti aongezewe likizo ya uzazi?

Katika majibu yake Naibu Waziri Mhe. Katambi amesema Haki ya Likizo ya Uzazi kwa mwanamke mwajiriwa ipo kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Sura ya 366, Marejeo ya Mwaka 2019 Kifungu cha 33 ambapo mwajiriwa mwanamke akijifungua mtoto mmoja anapewa likizo ya Uzazi ya siku themanini na nne (84) na akijifungua watoto mapacha hupewa siku mia moja (100), kadhalika akijifungua mtoto njiti hupewa siku 84 katika mzunguko wake wa likizo.

Naibu Waziri Mhe. Katambi ameendelea kufafanua kuwa uzoefu unaonesha kuwa wafanyakazi wanawake wanapewa likizo ya uzazi kwa mujibu wa Sheria na endapo likizo itamalizika na bado kuna uhitaji wa kumlea mtoto njiti, mwajiriwa anapaswa kujadiliana na mwajiri wake na kukubaliana kuhusu nyongeza ya likizo.

Ameongeza kuwa, mzazi anapokuwa amelazwa hospitalini akiwa na mtoto, anapaswa kupewa “Exemption from Duty” (ED) ambayo itamwezesha mwajiriwa huyo kuendelea kulea mwanaye bila kupoteza haki ya kulipwa mshahara wake endapo atawasilisha cheti cha daktari kwa mwajiri wake.

“Kwa Kuwa Sheria haijaainisha utaratibu mahususi wa kumwezesha mwanamke mwajiriwa kupewa likizo ya uzazi baada ya kujifungua mtoto njiti,ninapenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa, Ofisi yangu imelipokea suala hili na italifanyia kazi kwa kufanya maboresho katika kanuni za Sheria husika kuwawezesha waajiri kuandaa Sera za ajira ambapo pamoja na mambo mengine suala la likizo kwa mwanamke atakaye jifungua mtoto njiti litaanishwa kwa lengo la kumlinda mtoto njiti na mzazi wake”

Akijibu swali la nyongeza ,Naibu Waziri wa Afya,Dkt.Godwin Mollel amesema katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 vituo 100 vya watoto njiti vitajengwa .