News
Ndejembi aagiza mifumo ya fursa za vijana kusomana
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo ya kidijitali ya Serikali inayotoa taarifa za ajira na fursa kwa vijana kusomana ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
Amesema hayo baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano pamoja na Taasisi zake katika Maonesho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Mhe. Ndejembi amesema kuwa Serikali ni moja, hivyo ni muhimu mifumo ya Serikali iliyopo katika Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano na Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana kuunganishwa ili iweze kusomana na kubadilishana taarifa kwa urahisi.
“Serikali ni moja, tunatakiwa mifumo ya wizara zote isomane ili fursa zote tuzikusanye pamoja na kisha tuzipeleke kwa vijana wa Kitanzania,” amesema Mhe. Ndejembi.
Halikadhalika Mhe. Ndejembi, amesema kuwa muda alioutoa kwa ajili ya kutekeleza maelekezo aliyoyatoa jijini Arusha Septemba 28, 2026, kuhusu kuunganisha mifumo hiyo umepita. Hivyo, Serikali itaziita wizara zenye dhamana ya masuala hayo kwa ajili ya kikao cha pamoja kitakacholenga kujadili namna ya kupata suluhisho.

