Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

OSHA YAPONGEZWA KWA KUSIMAMIA VYEMA MASWALA YA USALAMA NA AFYA SEHEMU ZA KAZI


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeipongeza Taasisi ya Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kwa kusimamia vyema masuala ya Usalama na Afya katika maeneo ya kazi mbalimbali nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Najma Giga wakati walipofanya ziara ya kikazi na wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) na baadhi ya Maeneo ya Kazi Jijini Dar Es Salaam.

Mheshimiwa Najma Giga amesema kuwa Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazohusika moja kwa moja na uwezeshaji wa biashara nchini, hivyo kusimamia vyema maswala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi imekuwa ni chachu ya kuongeza fursa za uwekezaji nchini kutokana na uwepo wa mazingira rafiki ya Uwekezaji.

“Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Taasisi hii ya Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), mnatambua kwa maendeleo tunayoyatarajia kwenye taifa letu taasisi hii inaumuhimu mkubwa katika kusimamia maswala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi,” alisema Mheshimiwa Giga

Aliongeza kuwa taasisi hiyo imeboresha utendaji wake ukilinganisha na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma, hivyo alipongeza taasisi hiyo kwa kazi nzuri ambayo inaitekeleza ikiwemo kusimamia uslama na afya kwenye maeneo ya kazi.

Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imekuwa na mchango mkubwa sana kwa Taasisi ya OSHA kutokana na Miongozo na maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na kamati hiyo katika kuimarisha usalama na afya kwenye maeneo mbalimbali ya kazi nchini.

“Mafanikio haya ni utekelezaji wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha tunatengeneza mazingira bora na rafiki ya uwekezaji nchini,” alisema Waziri Mhagama

Alifafanua kuwa usajili wa sehemu za kazi umeongezeka kwa asilimia 119 ambapo ongezeko hilo limekuwa sambamba na kuongezeka kwa kaguzi pamoja na uchunguzi wa afya za wafanyakazi waliopo kwenye maeneo mbalimbali ya kazi.

Sambamba na hayo alielezea namna Serikali ilivyoridhia hoja ya kufanya marekebisho kupitia GN 719 ya tarehe 16 Novemba, 2018 kwa kuondoa tozo saba (7) ambazo zimepelekea ongezeko kubwa la sehemu za kazi kusajiliwa zaidi.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA), Bi. Hadija Mwenda alieleza kuwa ofisi hiyo imejipanga kuongeza uwajibikaji na kuimarisha mifumo ya usimamizi katika maeneo ya kazi ili kuleta tija zaidi katika kusimamia usalama na afya kwenye maeneo ya kazi.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi hiyo kwa namna inavyoshughulikia sekta ya kazi nchini sambamba na kufanya mageuzi makubwa katika mifumo na taratibu za kiutendaji iliyopelekea kuboresha suala zima la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Katika ziara hiyo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ilitembelea Kiwanda cha Sigara Tanzania (TCC) pamoja na Kiwanda cha Knuf kinachozalisha Gypsum katika eneo la Mkuranga.