Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Sangu: Ahmadiyya ni chachu ya amani, umoja na maendeleo ya taifa


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amekutana na Amiri na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania, Sheikh Khawaja Muzaffar Ahmad, pamoja na ujumbe wake, tarehe 16 Novemba 2026, Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Sangu ameipongeza Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania kwa mchango wake katika kuimarisha amani, upendo, mshikamano na maendeleo ya jamii kupitia mafundisho ya dini pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii nchini.

Naye, Sheikh Ahmad alitoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa ushirikiano na mazingira wezeshi yanayoendelea kutolewa kwa Jumuiya hiyo katika kutekeleza shughuli zake nchini.

Aidha, alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwake nchini mwaka 1934, Jumuiya hiyo imefanikiwa kuanzisha matawi 450 katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku ikiendelea kutekeleza jukumu lake la kueneza mafundisho ya Dini ya Kiislamu kwa kuzingatia misingi ya Qur'an Tukufu.

Kupitia mafundisho hayo, Jumuiya imekuwa ikihamasisha na kuimarisha tunu za amani, upendo, udugu, uvumilivu na heshima, pamoja na kuhimiza huduma kwa binadamu wote bila kujali tofauti za kabila, dini, imani au itikadi.

Akielezea mchango wa Jumuiya katika maendeleo ya jamii, Sheikh Ahmad alitaja miradi na programu mbalimbali za kurejesha kwa jamii (Community Development and Social Welfare Initiatives) zinazotekelezwa na Jumuiya hiyo. Miradi hiyo ni pamoja na kuanzisha na kuendesha hospitali pamoja na shule za msingi na sekondari mkoani Morogoro; kuanzisha chuo cha mafunzo ya ufundishaji wa dini kwa wazawa; na kuchimba visima vya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini.

Alieleza kuwa hadi sasa Jumuiya imefanikiwa kuchimba visima 500, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama, hususan kupitia kampeni ya Kumtua Mama Ndoo Kichwani.

Vilevile, alitaja mradi wa kuendeleza Kijiji cha Kisasa katika Mkoa wa Geita, unaolenga kuchochea maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi. Kwa ujumla, miradi hiyo inaonesha dhamira ya Jumuiya ya kuchangia ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa, sambamba na juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii na fursa bora za kiuchumi.

Mwisho.