Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

​Sangu: Sekta binafsi tengeni nafasi za mafunzo ya utarajali


✅ Serikali kuwezesha vijana 10,000 fursa za mafunzo kwa vitendo Serikalini

✅Ahamasisha Sekta Binafsi kutoa fursa za Mafunzo ya UtarajaliNa; OWM (KAM) - Dar es Salaam

Serikali imehamasisha Waajiri wa Sekta binafsi kutenga nafasi za mafunzo ya Utarajali (Internship) kwa wahitimu ili kuwawezesha kupata ujuzi na uzoefu unaohitajika katika soko la ajira, hatua itakayochangia kuongeza uwezo wao wa kumudu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Amebainisha hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu leo (Jumatatu tarehe 26 Oktoba, 2026) wakati wa mkutano na waajiri wa sekta binafsi kuhusu mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu uliofanyika jengo la ukumbi wa NSSF, Ilala Dar es Salaam.

Mhe. Sangu amesema kuwa, Mafunzo ya Utarajali yanapaswa kuwa daraja linalounganisha elimu na ajira, na kwamba kuongeza fursa hizo kutachangia kuwaandaa vijana kuajirika, kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa, sambamba na juhudi za kufikia lengo la kuzalisha ajira milioni nane ifikapo mwaka 2030.

“Waajiri wanahitaji watu wenye maarifa ya kitaaluma na uwezo wa kuyatumia kwa vitendo., hivyo mafunzo ya uzoefu wa kazi yanaunganisha maarifa ya darasani na utekelezaji wa majukumu halisi kazini kwa kusaidia wahitimu kutambua uwezo wao na maeneo wanayopaswa kuboresha,” amesema Waziri Sangu.

Kadhalika, Mhe. Sangu amesema Serikali imeweka lengo la kuwawezesha wahitimu 10,000 kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi katika kipindi cha mwaka wa fedha 2026/2027 pamoja na kufanikisha mpango wa kushirikiana na waajiri wa sekta binafsi katika kuwezesha fursa kwa wahitimu 20,000 kila mwaka.

Vilevile, amewataka waajiri kuhakikisha wahitimu wanapangiwa idara na vitengo vinavyoendana na fani walizosomea, kuwapatia mazingira salama ya kujifunzia, majukumu yenye malengo yanayopimika, na kuwapatia kipaumbele katika nafasi za ajira pindi zinapopatikana.

Kwa upande mwengine, Waziri Sangu amesema ushiriki wa waajiri wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha azma hiyo, akibainisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inatarajia sekta hiyo kuchangia takribani asilimia 70 ya utekelezaji wa dira hiyo.

Naye, Naibu Katibu Mkuu - Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) Bi. Zuhura Yunus amesema Serikali inaendelea kuratibu upatikanaji na utangazaji wa fursa za ajira na mafunzo kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Kazi Portal, pamoja na kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya maendeleo ya wahitimu wanaopata mafunzo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri nchini (ATE) Suzanne Ndomba-Doran amesema kuwa chama hicho cha Waajiri kimekuwa kikitumia kigezo cha waajiri wanaotoa fursa za mafunzo tarajali kama kigezo cha waajiri kupatiwa tuzo ya mwajiri bora wa mwaka.

Bi. Ndomba ameongeza kusema mwishoni mwa mwaka huu chama hicho kitaandaa tuzo bora kwa waajiri ikiwemo kuwatambua wale wanatengeneza fursa za mafunzo kwa vitendo kwa vijana wengi.

Mwakilishi wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Gasper Mdee amesema Shirikisho hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha vijana wanaohitimu nchini kunufaika na mafunzo hayo ya Utarajali hususani kwa waajiri wa sekta binafsi.

Akizungumza kwa naiba ya wanufaika wenzake, Bw. Gabriel Hugo, mnufaika wa mfumo wa mafunzo ya utarajali unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, amesema mfumo huo umemsaidia kubadili maisha yake baada ya kupata fursa ya mafunzo na hatimaye kuajiriwa kama Afisa wa Masoko katika Benki ya NBC. Amesema baada ya kujisajili kupitia mfumo wa Kazi Portal(zamani TaESA), aliitwa na kushiriki usaili mara mbili, hatua iliyomwezesha kupata nafasi ya mafunzo ya utarajali na baadaye kuajiriwa na benki hiyo.