Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Sangu: Ushirikiano wa Serikali na vyama vya wafanyakazi ni msingi wa Dira 2050


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (Mb), amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Serikali, vyama vya wafanyakazi na waajiri katika kujenga mazingira bora ya kazi na kuimarisha uchumi wa Taifa, kwani wadau hao ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema Serikali itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa waajiri na vyama vya wafanyakazi katika kuweka mazingira bora ya kazi yatakayochochea maendeleo ya Taifa.

Mhe. Sangu amesema hayo Novemba 11, 2026, wakati akifungua semina ya waajiri na viongozi wa matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeweka msisitizo katika kuoanisha shughuli za maendeleo na usimamizi wa masuala ya kazi na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

"Dira ya 2050 inalenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaotegemea rasilimali watu yenye ujuzi, nidhamu na tija kubwa, ambapo wafanyakazi ni moja ya nguzo kuu katika kufikia azma hii," amesema.

Kadhalika, amesema Serikali imeweka mikakati thabiti kupitia Mwongozo wa Majadiliano wa Mwaka 2025 baina ya Serikali, vyama vya wafanyakazi na vyama vya waajiri, unaotoa fursa kwa pande hizo kujadiliana kwa amani badala ya kuingia katika mivutano isiyo na tija.

Waziri Sangu ametoa wito kwa waajiri kuruhusu kuanzishwa kwa mabaraza ya kazi katika maeneo yao ya kazi. Sambamba na hilo, amevitaka vyama vya wafanyakazi kuungana na kuondoa tabia ya kubaguana, akisisitiza kuwa msingi wa kuanzishwa kwa vyama hivyo ni kuunganisha nguvu za wafanyakazi wote bila ubaguzi.

Vilevile, amewasisitiza waajiri na vyama vya wafanyakazi kuhakikisha michango katika mifuko ya hifadhi ya jamii inawasilishwa kwa wakati na kuzingatia sheria na kanuni za kazi.

Naye Katibu Mkuu wa TUGHE, Rugemalira Rutatina, amesema chama hicho kimeendelea kuhimiza wafanyakazi na wanachama wake kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa ili kuongeza tija na ufanisi katika maeneo yao ya kazi, pamoja na kuepuka kuchochea migogoro isiyo ya lazima.

Katibu Mkuu huyo ameipongeza Serikali kwa namna inavyoshughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi nchini. "Tunaishukuru sana Serikali kwa kuzipatia ufumbuzi hoja nyingi zilizokuwa zikiwakabili wafanyakazi wa Tanzania kwa miaka kadhaa iliyopita. Kushughulikiwa kwa hoja hizo kumesaidia kuongeza ari na uwajibikaji wa wafanyakazi nchini," amesema Rutatina.

Mwisho.