News
Sangu: Wamiliki Viwanda Toeni Ushirikiano OSHA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu amewataka wamiliki wa viwanda nchini kuzingatia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ili kulinda ustawi wa wafanyakazi na kuongeza tija ya uzalishaji.
Waziri Sangu ametoa wito huo (Januari 05, 2026) mkoani Mwanza, wakati wa ziara yake maalum ya kukagua utekelezaji wa masuala ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi katika Kiwanda cha Omega Fish Limited.
Akiwa kiwandani hapo Waziri Sangu amepongeza menejimenti ya kiwanda hicho kwa kutoa ajira kwa wazawa na kuzingatia kwa vitendo sheria, kanuni na taratibu za usalama na afya mahali pa kazi.
Sambamba na hayo, Sangu amevitaka viwanda vyote nchini kushirikiana kwa karibu na Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) ili kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama, yenye tija na yanayochangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Awali akizungumza Mkurugenzi Mkuu OSHA, Khadija Mwenda alisema OSHA itaendelea kusimamia wamiliki wa viwanda nchini kutekeleza sheria ya usalama mahala pa kazi katika ili kuwawezesha wafanyakazi na waajiri kutumia muda mwingi katika shughuli za uzalishaji wenye tija.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Omega Fish Market Hamad Alsalman ameishukuru Serikali na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali katika kutekeleza majukumu ya kuhakikisha usalama mahala pa kazi unazingatiwa kisheria.
