News
Serikali yasisitiza Mapambano dhidi ya Utumikishaji wa Watoto
Serikali imezitaka sekta zote nchini kuimarisha ushirikiano katika kutokomeza utumikishwaji wa watoto, ikieleza kuwa vitendo hivyo vinawanyima watoto haki zao za msingi za elimu, malezi bora na maendeleo ya vipaji.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Watoto yanayofanyika kila Mwaka, siku na tarehe 12 Juni chini ya kauli mbiu isemayo, “Red Card to Child Labour: Fair Play for Children, Decent Work for Adults.”
Ameeleza kuwa utumikishwaji wa watoto ni kosa la kisheria lililopigwa marufuku kupitia Kifungu cha 5 cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura ya 366. Mbali na kuwanyima watoto haki zao, vitendo hivyo pia huathiri maendeleo ya kiuchumi ya familia na Taifa kwa kupunguza uwezo wa watoto kuendeleza vipaji na mchango wao wa baadaye katika uchumi.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imeendelea kutekeleza sera na mikakati mbalimbali ikiwemo Sera ya Elimu ya mwaka 2014 toleo la 2023 pamoja na Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Mtoto wa mwaka 2025/26 hadi 2029/30. Kupitia mkakati huo, Serikali inalenga kupunguza kiwango cha utumikishwaji wa watoto kutoka asilimia 25.8 mwaka 2024 hadi kufikia asilimia sifuri mwaka 2030.
Aidha, Serikali imepongeza mchango wa wadau mbalimbali ikiwemo mradi wa ECLA (Eliminating Child Labour in Agriculture) kwa kusaidia kuandaa Mwongozo wa Kazi katika Kilimo unaolenga kuzuia utumikishwaji wa watoto katika sekta ya kilimo. Juhudi hizo zimechangia kuongeza uelewa kwa wakulima na kusaidia kupunguza utumikishwaji wa watoto katika mazao ya tumbaku, mkonge, chai na pamba.
Wakati huo huo, Serikali imewahimiza wadau wa sekta za uvuvi, madini, biashara na kilimo biashara kuungana katika mapambano dhidi ya utumikishwaji wa watoto. Pia imetoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wadau wa utatu wakiwemu ATE na TUCTA kwa mchango wao katika kulinda haki za watoto na kuimarisha mazingira ya kazi yenye staha nchini.
