News
Tanzania, ILO kuendeleza ushirikiano katika sekta ya kazi
Tanzania imeahidi kuendeleza ushirikiano na Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika kukuza ajira zenye staha, kulinda haki za wafanyakazi na kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii.
Hayo yamesemwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina, tarehe 16 Novemba, 2026
jijini Geneva, Uswisi wakati wa Kikao cha 358 cha Bodi Magavana ya ILO kilichoambatana na zoezi la uchaguzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo ambapo Bw. Gilbert F. Houngbo, aliibuka mshindi kwa kipindi cha pili cha miaka mitano.
Mhe. Houngbo, raia wa Togo, amechaguliwa tena baada ya kupata kura 51 kati ya 56 zilizopigwa. Kipindi cha pili cha uongozi wa Mhe. Houngbo kitaanza Oktoba 1, 2027.
Katika kikao hicho, tamko la Tanzania lilisomwa na Mhe. Mlyambina alieleza dhamira ya Tanzania kuendelea kumpa ushirikiano Mkurugenzi Mkuu huyo katika kutekeleza programu na mikakati ya ILO, hususan katika kukuza ajira zenye staha, kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii, kuboresha mazingira ya kazi na kulinda haki za wafanyakazi.
Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho unaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina, ambaye aliambatana na Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa pamoja na viongozi na watendaji wa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
