Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Vijana wavutiwa na Kilimo kupitia Mafunzo ya Uanagenzi


Kilimo kimeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania kwa kutoa ajira, malighafi za viwandani na uhakika wa upatikanaji wa chakula. Hata hivyo, kwa miaka mingi sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya vijana wengi kutokuwa na hamasa ya kujihusisha na shughuli za kilimo, ambapo hali hiyo inaendelea kubadilika kutokana na utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa Nguvu Kazi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi.

Kupitia programu hiyo, vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini wamepata fursa ya mafunzo ya uanagenzi katika fani mbalimbali ikiwemo kilimo kwa lengo la kuwapatia ujuzi wa vitendo unaowawezesha kujiajiri, kuajiriwa ili kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.

Miongoni mwa vijana wanufaika na mafunzo ya Uanagenzi katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mamtukuna fani ya kilimo wameeleza kuwa mafunzo hayo yamebadilisha mtazamo wao kuhusu sekta ya kilimo na kuwafanya kuona fursa nyingi za kiuchumi zilizopo.

Mmoja wa wanafunzi wa uanagenzi katika fani ya kilimo, Timon Swai, amesema kupitia elimu anayopata sasa ameweza kujifunza mbinu bora za kilimo cha mbogamboga zinazomuwezesha kuongeza uzalishaji na kupata kipato. Timon ameishukuru Serikali kwa kuwapatia vijana mafunzo hayo ambayo yanafungua fursa za ajira na kuwasaidia kujitegemea.

Aidha, mwanafunzi mwingine wa uanagenzi, Sara Tesha, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kupata ujuzi wa matumizi ya viatilifu na mbolea za asili, mbinu sahihi za umwagiliaji na namna ya kuongeza uzalishaji wa mazao kwa tija kubwa, maarifa ambayo yatachangia kuongeza uzalishaji na kipato kwa vijana wengi.

Naye, Mkuu wa Chuo Bw. Mjengelaungu ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano kwa kuendelea kuwezesha programu za mafunzo ya uanagenzi zinazowasaidia vijana kupata stadi za kazi na kujitegemea kiuchumi. Ameeleza kuwa programu hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa vijana wengi kwani imewajengea uwezo wa kujiajiri pamoja na kushiriki katika maendeleo ya Taifa kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo ya Uanagenzi chuoni hapo, Bw. Innocent Mtei, amesema vijana wengi waliokuwa hawana ajira sasa wameanza kupata matumaini mapya kupitia mafunzo hayo. Amefafanua kuwa programu ya uanagenzi imekuwa ikiwapatia vijana maarifa, uzoefu na stadi zinazowawezesha kujitegemea badala ya kuendelea kutegemea familia zao.

Naye Mwalimu wa fani ya kilimo, Thobista Macha, amesema kilimo kina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha. Ameeleza kuwa vijana wanaopata mafunzo hayo hujifunza mbinu bora za kilimo cha kisasa zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji, kujiajiri na hata kuwaajiri wengine mara baada ya kuhitimu mafunzo yao.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kutekeleza programu mbalimbali za mafunzo ya stadi na uanagenzi kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini. Kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi pamoja na vyuo vingine za mafunzo, Serikali inalenga kuwaandaa vijana wenye ujuzi na ubunifu watakaoweza kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo na maeneo mengine ya uzalishaji mali ili kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.

MWISHO