News
Waajiri wahimizwa kuwekeza katika Afya za Wafanyakazi
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Dkt. Evaline Munisi amewataka Waajiri nchini kuwekeza katika Afya na Ustawi wa Wafanyakazi kuwa sehemu ya mikakati yao ya biashara ili kuongeza tija, ubunifu na ushindani, badala ya kuchukulia suala hilo kama jukumu la mara moja.
Dkt. Munisi alitoa wito huo wakati akifungua Bonanza la Tano la waajiri, Afya Bonanza lililoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Oktoba 24 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Amesema uwekezaji katika afya za wafanyakazi ni msingi wa kujenga nguvu kazi yenye uwezo, ari na ufanisi, hali inayochangia kukuza biashara na kuharakisha maendeleo ya taifa.
Kaulimbiu ya bonanza hilo kwa mwaka huu, ‘Invest in Health, Unlock Potential: Going the Extra Mile’, ambayo inakumbusha kwamba kuwekeza katika afya ya wafanyakazi ni kuwekeza katika nguvu kazi, ushindani wa biashara na maendeleo ya taifa.” Amesema Dkt. Munisi
Ameongeza kuwa kupitia michezo washiriki wanapata fursa ya kufahamu hali zao za kiafya mapema, uchunguzi na elimu ya afya, kujenga tabia ya kufanya mazoezi na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Aidha, shughuli hizo pia husaidia kuimarisha afya ya akili, kupunguza msongo wa mawazo na kujenga mahusiano mazuri kati ya wafanyakazi na waajiri, jambo linachochea ushirikiano katika maeneo ya kazi, kupunguza utoro, ajali na gharama zinazotokana na matibabu au kushuka kwa uwezo wa kufanya kazi.
Katika hatua nyingine amewaasa waajiri kuwashirikisha wafanyakazi katika kubuni na kutekeleza programu za afya na ustawi ili kuhakikisha zinakidhi mahitaji yao na kuleta matokeo endelevu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Bi. Suzan Ndomba amesema chama kinaendelea kushirikiana na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika kuwakumbusha waajiri umuhimu wa kulinda afya za Wafanyakazi.
Bonanza hilo la mwaka huu limewakutanisha waajiri, wafanyakazi na wadau wa sekta mbalimbali kwa ajili ya michezo, mazoezi na shughuli za kuhamasisha afya na ustawi mahali pa kazi.
