Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Wabunge Wapigwa Msasa Juu ya Kikokotoo Kipya


Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 29 Juni, 2022 wamepatiwa semina kuhusu kanuni mpya ya kikokotoo iliyotangazwa na Serikali hivi karibuni.Semina hiyo ni kufuatia maelekezo ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson aliyoyatoa tarehe 24 Juni, 2022 wakati Serikali ikihitimisha mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali.

Lengo la semina hilo ilikuwa ni kuwajengea uelewa wabunge kuhusu kanuni mpya za mafao ambazo zitaanza kutumika rasmi tarehe 1 Julai, 2022.

Katika Semina hiyo wasilisho la Kikokotoo kipya liliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (Mb) na kuongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu.

Naye, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Zungu alipongeza kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau ambao ni TUCTA na ATE katika kuanda kanuni mpya za mafao ambapo sasa zitakuwa ni asilimia 33.

“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha haki za wafanyakazi zinazingatiwa pia tunampongeza Mhe. Profesa Ndalichako na Mhe. Jenista Mhagama pamoja na wadau wote kwa kazi kubwa waliyofanya,”

Kwa upande wao rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran wa nyakati tofauti walisema viongozi wa vyama vya wafanya kazi ambao ni wadau muhimu walishiriki hatua zote katika mchakato wa kuanda kanuni mpya za mafao na wameridhia kuanza kutumika kwa kikokotoo kipya.

Wakichangia katika Semina hiyo, wabunge wameipongeza serikali kwa kuwezesha kuleta ulinganifu wa mafao ya mkupuo na pensheni ya mwezi kwa watumishi wote wa sekta Binafsi na Umma. Aidha, wamepingeza Kikokotoo hicho kwa kuwa kitajenga mifuko imara na endelevu.

Wakitoa ufafanuzi juu ya masuala yaliyoibuka katika semina hiyo kutoka kwa baadhi ya wabunge, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kishimba wamewahakikishia wabunge kuwa mifuko hiyo itaendelea kulipa mafao ya mkupuo na pensheni kwa wakati kwa wanachama.