News
Waziri Mkuu Ahimiza Watanzania Kuwatunza Watoto wenye Uhitaji
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Lameck Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kushirikiana na Serikali kutunza na kuhudumia vituo vya watoto wenye mahitaji maalumu na wasiojiweza badala ya kutegemea wahisani au misaada ya nje, akisisitiza kuwa jukumu hilo linapaswa kubebwa na Watanzania wenyewe kupitia rasilimali za ndani.
Dkt. Nchemba amesema hayo leo Juni 21, 2026 katika harambee iliyoandaliwa na Kanisa la Anglikana Tanzania, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejielekeza katika kujenga uchumi unaotegemea mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ya nchi.
Amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuwa na bajeti inayotegemea mapato ya taifa badala ya misaada, huku akiwataka Watanzania kuachana na dhana iliyozoeleka ya kwamba vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji vinaendeshwa kwa misaada kutoka nje au kwa kutegemea wasamaria wema pekee.
"Wajibu wa kuwahudumia watoto yatima na wenye mahitaji maalum ni wetu kama Watanzania. Serikali imekwishatoa miongozo kwa mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinakuwa na orodha za watoto wenye uhitaji ili wajibu huo utekelezwe ipasavyo," amesema Waziri Mkuu
Ameongeza kuwa bajeti ya Kuu yw Serikali ya mwaka 2026/2027 imejengwa kwa kuzingatia mapato ya ndani yanayotokana na kodi na vyanzo vingine vya mapato ya taifa, hatua inayodhihirisha dhamira ya kujitegemea katika kugharamia maendeleo na huduma za kijamii.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amepongeza Kanisa kwa mchango wake mkubwa wa kiroho na kijamii, akisema kazi ya kuhubiri Injili, maombi na mafundisho ya maadili imekuwa nguzo muhimu katika kuimarisha ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.
Vilevile, amesema Serikali inatambua mchango wa taasisi za dini katika kujenga jamii yenye maadili mema, mshikamano na amani, hali inayowezesha shughuli za maendeleo kufanyika kwa utulivu.
Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhimiza na kusimamia masuala ya umoja wa kitaifa, haki na amani ili wananchi waweze kutekeleza shughuli zao za ibada na maendeleo katika mazingira tulivu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuanzisha Idara ya Mahusiano inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, na kueleza kuwa idara hiyo imeendelea kuimarisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Kadhalika, ameahidi Serikali itaendelea kuwaleta Watanzania pamoja na kusimamia kwa vitendo maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha yanatekelezwa kwa ufanisi ili kuimarisha maendeleo, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mhashamu Maimbo Mndolwa, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwake, Kanisa la Anglikana limeendelea kuongozwa na misingi mitatu muhimu ambayo ni Maandiko Matakatifu, mapokeo ya Kanisa pamoja na matumizi sahihi ya akili katika kutafsiri na kutekeleza mafundisho ya dini kwa manufaa ya waumini na jamii kwa ujumla.
Askofu Mndolwa amesema misingi hiyo imekuwa dira muhimu katika kuimarisha huduma za kiroho, maadili na maendeleo ya kijamii, huku Kanisa likiendelea kushirikiana na Serikali katika kuchochea maendeleo ya Taifa.
Aidha, amemshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo na kuipongeza Kamati ya Maandalizi pamoja na wadau wote waliochangia kufanikisha tukio hilo. Alisema harambee hiyo inalenga kukusanya Shilingi bilioni 1.5 ambazo zitatumika kuanzisha na kuendeleza kitega uchumi cha Kanisa, hatua itakayoliwezesha Kanisa kuimarisha huduma zake za kiroho na kijamii kwa manufaa ya waumini na jamii kwa ujumla.
MWISHO.
