Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Bulyankulu yapongezwa kwa kuwekeza mifumo ya usalama wa wafanyakazi mgodini


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii umeupongeza Mgodi wa Bulyanhulu kwa kuwekeza kwenye mifumo ya Usalama na Afya wa wafanyakazi ili kuhakikisha wafanyakazi wanalindwa dhidi ya vihatarishi.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Chakoma, wakati wa ziara ya kamati katika eneo la mgodi wa Bulyanhulu wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga, iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa sheria namba 297 ya mwaka 2023 inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, kuhusu Usalama na Afya mahali pa kazi.

Mhe. Chakoma amesema kamati hiyo imefanya ziara hiyo ili kutathmini namna wafanyakazi wanavyolindwa dhidi ya vihatarishi vinavyotokana na shughuli za uchimbaji wa madini, pamoja na namna mifumo ya kuwasaidia wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kudhibiti ajali au magonjwa wakiwa kazini.

“Tunataka kuona ni kwa namna gani wenzetu wa mgodi wanajaribu kuondoa vihatarishi kwa wafanyakazi, au kuwahudumia wanaopata changamoto hizo wakiwa mahali pa kazi, na tunatambua sehemu zenye Migodi zina vihatarishi vingi endapo visivyodhibitiwa vinaweza kuleta madhara makubwa” amesema Bi. Chakoma.

Aidha Mwenyekiti huyo ameungana na wajumbe wengine wa kamati hiyo ya bunge kuipongeza OSHA kwa namna inavyosimamia masuala ya usalama na afya hapa nchini, akitolewa mfano maeneo ya migodi jinsi, masuala ya usalama na Afya yanavyotekelezwa hapa nchini, ikiwemo ushauri uliotolewa na OSHA, na kupelekea migodi hio kuja matumizi ya teknolojia mbalimbali kupunguza ajali na magonjwa yanayoweza kupelekea vifo au ulemavu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, amesema kuwa Serikali kupitia OSHA imeendelea kufanya kaguzi na kutoa elimu ya Usalama na Afya mahali pa Kazi kwa wafanyakazi.

Naibu Waziri, Dkt. Munisi amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, jumla ya kaguzi 871 zilifanyika mkoani Shinyanga, huku wafanyakazi 7,969 wakifanyiwa vipimo vya afya mkoani humo.

Aidha, Naibu Waziri amesema kuwa waajiri 102 walikidhi matakwa ya sheria ya Usalama na Afya na kupatiwa vyeti vya ithibati, huku waajiri wengine wakipewa maelekezo ya kufanya maboresho katika maeneo yaliyobainika kuwa na changamoto.

Katika eneo la mafunzo, Dkt. Munisi amesema jumla ya wafanyakazi 931 walipatiwa mafunzo kuhusu usalama na afya mahali pa kazi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema kuwa OSHA inaendelea kusimamia usalama na afya mahali pa kazi kwa kuhakikisha waajiri wanaweka mifumo inayolinda usalama na afya za wafanyakazi huku ikiweka mkazo katika elimu na uhamasishaji ili waajiri waweze kutekeleza wajibu wao kwa uelewa.

Bi Khadija amesema OSHA, imeendelea kuhamasisha uwekezaji kwenye matumizi ya teknolojia kwa lengo la kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa salama.

Naye Kaimu Meneja wa Usalama na Afya wa Mgodi Bulyahulu Bw. Akida Waria amesema Mgodi huo umekuwa ukifanya vizuri katika masuala ya Usalama na Afya, na Kwa mwaka 2025/2026 hakukuwa na tukio lolote la ajali lilotokea eneo hilo.

Waria amesema mgodi huo umewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye teknolojia, hasa katika sehemu zenye hatari kubwa kufanywa na mashine hivyo kuondoa hatari zinazoweza kusababisha ajali kwa wafanyakazi

Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati ya Bunge, kufuatilia utekelezaji wa sheria pamoja na maelekezo wanayoyatoa wakati wa uwasilishaji wa taarifa kwenye kamati hio.