News
Waziri Sangu: Wahitimu Mafunzo ya Uanzagenzi kunufaika na vifaa mtaji
✅Wanagenzi 5,746 wanufaika na Mafunzo ya Uanagenzi mwaka wa fedha 2025/2026
Na. OWM (KAM) - Dar es Salaam
Vijana Wahitimu wa Mafunzo ya Uanagenzi Awamu ya Nane wamehimizwa kujiunga katika vikundi vya uzalishaji na ujasiriamali ili kuunganisha nguvu, rasilimali na ujuzi wao katika kuanzisha na kujiendeleza kupitia shughuli za kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu leo Novemba 27, 2026 wakati akihutubia katika mahafali ya 5 ya Chuo cha AnnaCollection Fashion Academy, yaliyofanyika East Africa Commercial & Logistic Center, Jijini Dar es Salaam.

Amesema, katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano inaendelea na jitihada za kuwawezesha wahitimu wa mafunzo hayo kupata vifaa vya mtaji kwa ajili ya kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi. kwa kuzingatia vigezo na taratibu zilizowekwa.
Vilevile amesema, katika kuimarisha ustawi wa wanagenzi, amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya mafunzo kwa kuwapatia bima ya afya pamoja na posho ya usafiri ya shilingi 100,000 kwa mwezi kwa kipindi cha miezi miwili wanapokuwa katika mafunzo ya vitendo.
“Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano inaendelea kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inatekelezwa kwa katika maeneo manne, yakiwemo Mafunzo ya Uanagenzi, Uzoefu wa kazi kwa wahitimu, kuendeleza ujuzi kwa wafanyakazi pamoja na urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo kwa lengo la kuandaa nguvu kazi yenye maarifa, ujuzi na umahiri unaoendana na mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia,” amesema

Kadhalika, amewataka vijana hao kutumia fursa mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi zinazotolewa na Serikali na taasisi za fedha ili kujenga na kukuza biashara zitakazowawezesha kujipatia kipato na kutoa ajira kwa Watanzania wengine.
Akizungumzia fursa katika sekta ya mitindo na mavazi, Mhe. Sangu amewahimiza wahitimu kutumia malighafi zinazopatikana nchini, ikiwemo pamba, kuongeza thamani ya bidhaa, kuanzisha biashara na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati, akieleza kuwa sekta hiyo ina mnyororo mpana wa thamani kuanzia uzalishaji wa malighafi, ubunifu, ushonaji hadi masoko na biashara.
Kwa upande mwengine, Waziri Sangu amewataka wahitimu kuthamini uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa kuwapatia ujuzi hivyo kutumia maarifa na ujuzi huo kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla. Pia, ameitaka Menejimenti ya AnnaCollection Fashion Academy kuendelea kuimarisha ubora wa mafunzo kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira, kujenga misingi ya maadili na nidhamu kwa wanafunzi pamoja na kuimarisha ushirikiano na waajiri ili kuongeza fursa za mafunzo kwa vitendo na ajira kwa wahitimu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Anna Collection Fashion Academy (AFA), Bi. Anna Lunguya amesema chuo hiko kilianzishwa kwa lengo la kuleta ubunifu katika fani ya ushonaji na mitindo ili kuongeza wigo wa Watanzania kujiajiri katika sekta hiyo ya mavazi, hivyo ameshukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kukiamini chuo hicho na kukipatia fursa ya kutoa mafunzo ya Uanagezi kwa vijana 126 ambao kati yao Wanagenzi 118 wameweza kuhitimu.

Akitoa shukrani kwa naiba ya wanafunzi waliohitimu, Clara Joachim ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kupata ujuzi ambao utawasaidia kujiajiri na kuendesha maisha yao bila ya kutegemea kuajiriwa.
