News
Bunge laipongeza NSSF kwa usimamizi bora wa Mfuko

Pongezi hizo zimetolewa Alhamisi ( Oktoba 15, 2026 ) jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu, wakati Kamati ilipopokea taarifa ya mwenendo wa NSSF katika kuwahudumia wanachama wa sekta binafsi.
Mhe. Mchafu ameitaka NSSF kuimarisha na kupanua wigo wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii, kwa kuzingatia makundi mbalimbali katika sekta zote za uzalishaji, hususan sekta rasmi.

Kamati pia imeipongeza Serikali kwa uamuzi wa kuondoa faini kwa waajiri waliochelewa kuwasilisha michango ya wafanyakazi, ikisema hatua hiyo inapunguza mzigo kwa waajiri na kuimarisha mazingira ya biashara.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema vipaumbele vya NSSF ni kupanua upatikanaji wa huduma jumuishi za hifadhi ya jamii kwa wananchi wote.
Sangu amesema NSSF inaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa kuzingatia Nguzo ya Pili ya Dira ya 2050 inayohusu uwezo wa watu na maendeleo.
Amesema Serikali na NSSF zinaendelea kutoa elimu kwa umma, ikiwemo kuanzishwa kwa Skimu ya Hifadhi ya Jamii iliyoboreshwa kwa waliojiajiri ili wanufaike kama wafanyakazi wa sekta rasmi.
Waziri huyo aliongeza kusema idadi ya wanachama wa NSSF imeongezeka kwa asilimia 65 kutoka 1,358,882 mwaka 2023/24 hadi 2,243,901 robo ya kwanza ya mwaka 2026/27, huku wanachama wa Skimu ya Hifadhi ya Jamii wakiongezeka kwa asilimia 357 kutoka 142,314 hadi 650,207.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, aliiambia Kamati kuwa mfuko umejipanga kuongeza wanachama kwa kuyafikia makundi maalumu yakiwemo mama lishe na wafanyabiashara wadogo.
Mushomba aliongeza kusema mkakati huo unalenga kuhakikisha waliojiajiri wanapata fursa ya kunufaika na huduma za hifadhi ya jamii ili kuimarisha ustawi na usalama wa kipato uzeeni.
Kamati hiyo ya Bunge inaendelea na vikao vyake ambapo tayari imekwishapokea taarifa za utendaji kazi ikiwemo Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na kesho itakutana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Mwisho.
