Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

WAJASIRIAMALI WA TZ WAISHUKURU SERIKALI KUWAWEZESHA KUSHIRIKI MAONESHO NCHINI RWANDA


WAJASIRIAMALI kutoka nchini Tanzania wanaoshiriki katika maonesho ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Juakali nchini Rwanda wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kushiriki maonesho hayo.

Wajasiriamali hao wamesema hayo Novemba 2, 2026 katika viwanja vya Gikondo Jijini Kigali, Rwanda.

Wamesema, ushiriki wao katika maonyesho hayo umekuwa fursa muhimu ya kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao, kukutana na wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali na kujifunza namna ya kuendesha shughuli zao kwa tija zaidi.

Akizungumza Mjasiriamali Bw. Paul Onesmo ambae ni mtengenezaji wa bidhaa za Ngozi amesema kuwa kupitia maonesho hayo wamepata nafasi ya kuonyesha bidhaa mbalimbali wanazozalisha, jambo lililowapa fursa ya kujitangaza katika soko la kimataifa na kuonyesha uwezo wa ubunifu walionao wajasiriamali wa Tanzania.

Naye, Mjasiriamali mwengine Bi. Janeth Geofrey amesema maonesho hayo wamejifunza teknolojia na mbinu mpya za uzalishaji kutoka kwa washiriki wengine, ambazo wanatarajia kuzitumia wanaporejea nchini ili kuboresha ubora wa bidhaa zao na kuongeza ushindani katika soko.

Kadhalika, Wajasiriamali hao wameiomba Serikali iendelee kuwaunga mkono kwa kuwapatia fursa zaidi za kushiriki maonyesho ya ndani na nje ya nchi ili wajasiriamali wengi zaidi waweze kunufaika na fursa za masoko na teknolojia .

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati katika Jumuiya ya Afrika Afrika Mashariki (CISO – Tanzania), Bw. Josephat Rweyemamu ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitria Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na MAhusiano kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wajasiriamali na kufanikisha kushiriki maonesho hayo

Amesema kuwa, CISO itaendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali ili kuendeleza ujuzi wa zaidi kwa wajasiriamali kwa lengo la kuendelea kuzalisha bidhaa zenye tija zinzoenda na soko la kimataifa.