News
Dkt. Nchemba apongeza Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi) Kujisogeza kwa Wananchi
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano kwa kazi inayofanywa na Ofisi hiyo pamoja na taasisi zake, akisema ushiriki wao katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026 ni fursa ya kujisogeza karibu zaidi na wananchi.
Pongezi hizo amezitoa baada ya kutembelea banda la Ofisi hiyo katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, ambako maadhimisho hayo yanafanyika.
Dkt. Nchemba amesema ushiriki wa Ofisi hiyo na taasisi zake katika maonyesho hayo ni fursa muhimu ya kuwafikia wananchi moja kwa moja, kuwapa taarifa kuhusu huduma zinazotolewa na kuongeza uelewa wa masuala ya kazi, ajira na hifadhi ya jamii.
Maadhimisho hayo yanashirikisha Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano pamoja na taasisi zake ambazo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
Kupitia taasisi hizo, wananchi hususan vijana wanapata taarifa kuhusu huduma mbalimbali, haki na wajibu kazini, usalama na afya mahali pa kazi pamoja na fursa za ajira na hifadhi ya jamii.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amewapongeza watumishi wa taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa elimu kwa wananchi. Amewasisitiza kuendelea kujenga na kudumisha mahusiano mema katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha utoaji huduma.
Naye Afisa Hifadhi ya Jamii kutoka Ofisi hiyo, Sohela Mabeyo, amemueleza Waziri Mkuu kuwa Ofisi inatekeleza Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi inayolenga kutoa mafunzo ya uanagenzi, kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi, kutoa uzoefu wa kazi kwa wahitimu na kurasimisha ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Amesema pia Ofisi inaratibu upatikanaji wa fursa za ajira ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na mawakala binafsi waliosajiliwa kisheria, huku akiwahimiza Watanzania hususan vijana kujisajili kwenye mfumo wa Kazi Portal ili kupata taarifa na kunufaika na fursa za ajira.
Waziri Mkuu yupo mkoani Rukwa kwa ajili ya kushiriki kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 kinachotarajiwa kufanyika Oktoba 14, 2026 mkoani humo.
Mbio za mwaka huu zinaongozwa na kaulimbiu isemayo, "Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo," inayohimiza umoja, mshikamano na ushiriki wa wananchi katika kuleta maendeleo ya Taifa.


