News
Dkt. Nchimbi ahimiza Viongozi wa dini kusimamia maadili
Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesisitizia Viongozi wa Dini kuendelea kusimamia maadili na kulinda Amani.
Dkt. Nchimbi amesema hayo leo wakati wa hafla ya Usimikaji na Uzinduzi wa Uongozi wa Awamu ya Tano wa The Council Of Pentecostal Churches Of Tanzania (CPCT) iliyofanyika katika Ukumbi wa Agape Life Church Mbezi Jogoo, Jijini Dar es salaam leo Tarehe 06 Februari 2026.
Dkt. Nchimbi ameongezea kuwa nia ya Serikali ni kuongeza ushirikiano mzuri na taasisi za Dini na kwa kipindi hiki Mahusiano ya Kanisa na Serikali yameimarika.
“Nataka kuwahikikishia kuwa Serikali itaendeleza ushirikiano na taasisi za Dini na ndio maana kipekee kabisa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliunda Wizara Maalum ya kushughulikia masuala ya Mahusiano na nimekuwa nikifatilia namna inavyotekeleza majukumu na nimefurahishwa na wizara hii”
Ameongeza kuwa, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi pamoja na Taasisi za Dini na Serikali inatambua Mchango Mkubwa unao tolewa na taasisi za dini katika jamii.
Akizungumza awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amesema katika kuratibu suala la Mahusiano, Serikali imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa kutaratibu suala hilo na utazinduliwa karibuni.
Naye, Mwenyekiti wa CPCT, Askofu Vernon Fernandes, ameshukuru Serikali kwa kuanzisha Idara ya Mahusiano ambayo imekuwa ikiwaleta pamoja viongozi wa dini.
